MGOMBEA wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) John Magufuli leo Jumatano Septemba 9, 2020, amewaambia wananchi wa Geita katika mkutano wa kampeni zake kwamba katika kipindi cha miaka mitano atatengeneza ajira milioni nane.
Pamoja na kauli hiyo, maneno mengine aliyoyasema kwenye kampeni hiyo ni:
“Kwa miaka mingi Geita tulikuwa na hifadhi moja tu ya Rubondo hivyo kwenye miaka mitano iliyopita tumeanzisha hifadhi nyingine mpya ya taifa ya Burigi, Chato, ambayo ni ya tatu kwa ukubwa Tanzania.
“Zamani ilikuwa ukishagundua dhahabu unafukuzwa wanakuja wakubwa, tukasema hapana wakigundua wanabaki palepale na wanapewa leseni na wao waweze kutajirika kwa sababu tunawahesabu wao kama wawekezaji.
“Tumejitahidi kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwatengea maeneo, kufuta ama kupunguza viwango vya kodi walivyokuwa wanalipa na kuwapatia mafunzo na mitambo ya kuendesha shughuli zao za uchimbaji.”



