MVUTANO unaendelea kati ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na vyama viwili vya siasa; Chama cha Demokrasiana Maendeleo (CHADEMA) na ACT-Wazalendo ambapo msajili akikemea kuungana kwa vyama kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu huku, na vyama hivyo vikisisitiza kutorudi nyuma katika azma yake ya kushirikiana.
Kwa takriban wiki moja sasa, kumekuwa na mvutano baina ya pande hizo mbili, ofisi ya msajili ikidai kuna uvunjaji wa sheria vyama kutaka kuungana, huku vyenyewe vikidai havijavunja sheria husika.
Wakati msajili asisitiza ofisi yake kutofumbia macho suala hilo, Chama cha ACT-Wazalendo jana kilisambaza kwa vyombo vya habari barua yenye kumbukumbu namba HA, 322/362/21/90 kiliyoiandika Septemba 22 mwaka huu kuijibu ofisi hiyo iliyokitaka kiwasilishe maelezo kuhusu mgombea wake wa urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, kudaiwa kumwombea kura mgombea wa urais wa Tanzania, Tundu Lissu.
Barua hiyo iliyoandikwa na Ofisi ya Katibu Mkuu wa chama hicho, ilirejea barua waliyoandikiwa na Ofisi ya Msajili ikiwakumbuha uwapo kwa Kifungu cha 11A cha Sheria ya Vyama vya Siasa kinachoweka utaratibu wa vyama kushirikiana na kukiuka ni kuvunja sheria.
“Tunapenda kueleza kuwa mgombea wetu wa urais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad, hajakiuka kifungu cha 11A cha Sheria ya Vyama vya Siasa, kinachoweka utaratibu wa vyama kuungana au vinavyokusudia kuungana kabla au baada ya uchaguzi,” inasomeka sehemu ya barua hiyo.
Chama hicho kupitia barua yake hiyo, kinadai kuwa Maalim Seif hakumwombea kura Lissu kama inavyodaiwa na Ofisi ya Msajili na kwamba kipande cha video iliyotumiwa hakina maneno ya kumwombea kura mgombea huyo.
“Alichokisema Maalim Seif ni imani yake kwa Lissu atakuwa Rais wa Tanzania jambo ambalo lipo wazi sana kutokana na mwelekeo wake wa kuungwa mkono na Watanzania walio wengi.
“Hili siyo kosa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa. Kwa maelezo hayo, ni matumaini yetu kuwa sasa utakuwa umefahamu maana ya tafsiri sahihi na tofauti ya vyama kuungana chini ya kifungu cha 11A cha Sheria ya Vyama vya Siasa na mgombea mmoja kuonyesha imani yake kwa mgombea mwingine katika uchaguzi huu,” ilielezwa zaidi katika barua hiyo ya ACT-Wazalendo.
Wakati ACT-Wazalendo wakiyasema hayo, CHADEMA kupitia kwa Katibu Mkuu wake, John Manyika, iliiambia Nipashe jana kuwa kinachoendelea kinawapa hisia za Ofisi ya Msajili kutumika kuviumiza baadhi ya vyama vya upinzani kwa kuwa hawajawahi kutangaza kuunda muungano wa vyama.
Alidai hawajakiuka kifungu cha 11A cha Sheria ya Vyama vya Siasa na kwamba kutaka mgombea wa chama kingine achaguliwe siyo kosa kwa mujibu wa sheria.
“Hatutarudi nyuma, suala hili tutatoa taarifa zaidi kupitia mkutano wetu na waandishi wa habari kesho (leo),” alisema Mnyika.
KAULI YA MSAJILI
Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, akihojiwa na BBC juzi, alisema hawataruhusu wagombea au vyama vilivyosimamisha wagombea, kuungana kwa sababu kufanya hivyo ni kuvunja sheria na kuwachanganya wananchi.
Alisema kabla ya kuanza kwa mchakato wa kampeni za uchaguzi, walikaa na viongozi wote wa vyama vya siasa na kuwaeleza mambo ya kuzingatiwa, lakini bado kuna vyama vinakiuka sheria na taratibu.
Alisema tayari wameshaviandikia barua CHADEMA na ACT-Wazalendo kuhusu ukiukwaji wa sheria unaodaiwa kufanywa na vyama hivyo.
“Mgombea wa CHADEMA, alimnadi wa ACT-Wazalendo, tumeshawaandikia barua na vilevile wa ACT-Wazalendo alimnadi mgombea wa CHADEMA, tumeshamwandikia barua. Tunaendelea kuchukua hatua. Kwanza, tulikutana nao kuwaasa kuzingatia sheria na hatutaruhusu kuvunja sheria,” alisema Nyahoza.
Mwanasheria Frugence Massawe akizungumzia suala hilo, alisema lina mkanganyiko kwa sababu Sheria Na. 1 ya Uchaguzi ya Mwaka 2019 kifungu cha 11A kinaeleza namna ya kuungana kuanzia hatua ya mchakato hadi kupeleka maombi yao kwa Msajili.
Alisema sheria hiyo iliyofanyiwa marekebisho mwaka jana, haijakataza ushirikiano wa vyama vya siasa usio rasmi.
Alitolea mfano ushirikiano usio rasmi ni mkutano mkuu wa ACT-Wazalendo kumwalika Tundu Lissu ambaye katika mkutano huo pia alipata fursa ya kuhutubia.
Alikumbusha kuwa hata mkutano mkuu wa CCM uliofanyika Dodoma mwaka huu ulialika vyama vingine vya siasa na kupewa fursa ya kutoa salamu zao.
“Hiyo ni mifano ya ushirikiano usio rasmi ambao sheria haijakataza ushirikiano kama huo,” alisema Massawe.
Mwanasheria huyo pia alirejea uamuzi wa Chama cha TLP wa kutangaza kumuunga mkono mgombea urais wa CCM, John Magufuli na kuweka bayana kuwa ndiye mgombea wa TLP, nao ni ushirikiano usio rasmi.
Alisema demokrasia nchini bado haijakua kama mataifa mengine ambayo vyama vinaweza kutangaza msimamo wake kuhusu mgombea anayeonekana kufaa na suala hilo siyo kosa kisheria.
