HATIMAYE kijana James Charles maarufu kwa jina la ‘James Delicious’ amelipiwa faini ya Tsh milioni 5 aliyokuwa amehukumiwa kulipa au kwenda jela miaka mitano baada ya kupatikana na kosa la kufanya mapenzi kinyume na maumbile.
Pay Slip ya benki ya CRDB inaonyesha kiasi hicho kimelipwa kupitia tawi la benki hiyo lililopo Azikiwe jijini Dar es Salaam jana Septemba 28, 2020, saa 7:23 mchana, hivyo kwa sasa ameachiwa na yupo huru.
Ikumbukwe kuwa, msanii Rutyfiya Abubakary maarufu kama ‘Amber Rutty’ na mpenzi wake Said Bakary ni watuhumiwa waliohukumiwa hivi karibuni kulipa faini ya jumla ya Tsh. Milioni 11 ama kutumikia kifungo cha miaka mitano jela kila mmoja baada ya kupatikana na hatia katika makosa matatu likiwemo kosa la kufanya mapenzi kinyume na maumbile.
Hata hivyo, washtakiwa wote hao, walishindwa kulipa faini hiyo na hivyo wamepelekwa gerezani.
Hukumu hiyo ilisomwa Septemba 25, na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambaye amesema, mahakama imewatia hatiani washtakiwa wote baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi kumi wa upande wa mashtaka ambao wameweza kuthibitisha makosa pasipo kuacha shaka yoyote.
