KAMPUNI ya Global Publishers inayojihusisha na uchapaji wa magazeti ya michezo ya Championi na Spoti Xtra, kwa kutambua kiu ya wasomaji wao kupata habari makini za michezo na burudani, kesho Jumanne inatarajiwa kufanya uzinduzi mkubwa wa gazeti jipya la michezo la Spoti Xtra Jumanne.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Usambazaji cha Global Publishers, Anthony Adam, alisema Spoti Xtra Jumanne ni gazeti jipya lililosheheni habari mbalimbali za michezo na burudani za hapa nyumbani Tanzania na nje ya mipaka ya nchi, zilizoandikwa na kuhaririwa na waandishi mahiri kwa ajili ya kukidhi na kukata kiu ya wanamichezo wote nchini.
“Kwa muda sasa tumekuwa mtaani kutangaza ujio mkubwa wa Gazeti la Spoti Xtra Jumanne ambalo linaingia mtaani Jumanne hii (kesho) kama sehemu ya mapendekezo ya wasomaji wetu kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini.
“Kama mnavyojua Global Publishers hapo kabla haikuwa na gazeti la michezo lililokuwa likitoka siku ya Jumanne hivyo kuwaachia wasomaji wetu kiu kubwa ya taarifa za kimichezo, hali hiyo iliusukuma uongozi wetu kuja na Spoti Xtra Jumanne ili kukidhi mahitaji ya wasomaji wetu,” alisema Adam.
MWANDISHI WETU, Dar es Salaam
