
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kuchukua usimamizi wa Benki ya Biashara ya China (China Commercial Bank Limited) ambayo ina tawi lake jijini Dar es Salaam nchini Tanzania kuanzia leo Novemba 19, 2020.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema hii leo jijini Dodoma, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga, amesema kutokana na mamlaka aliyopewa ya sheria za benki na taasisi za fedha, Benki Kuu imeamua kuchukua usimamizi wa benki hiyo ya China baada ya kushindwa kukidhi masharti ya kuwa na akiba ya kutosha ili kuweza kuendesha shughuli za kibenki.
Benki hiyo hivi sasa itakuwa chini ya uangalizi wa Benki Kuu ya Tanzania kwa muda wa siku 90, huku bodi yake ya wakurugenzi pamoja na menejimenti ikisimamishwa na huduma zote kwa wateja kusitishwa.