×

Rais Ramaphosa Amsaka Aliyemtorosha Nabii Bushiri

RAIS wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, amesema kuwa kutoroka kwa Nabii wa Malawi na mke wake nchini humo ni jambo ambalo analifuatilia kwa karibu na ameahidi kuchukua hatua baada ya kupata taarifa za kina.

 

Nabii Shepherd Bushiri na mke wake Mary, wanakabiliwa na mashtaka ya ulaghai na utakatishaji wa fedha nchini Afrika Kusini. Wawili hao walitoroka nchini Afrika Kusini wiki iliyopita na kujisalimisha polisi nchini Malawi baada ya Afrika Kusini kutoa kibali cha kukamatwa kwao.

 

Rais Ramaphosa amesema kupitia televisheni kwamba tukio la wawili hao kutoroka “Halikutakiwa kutokea. Bila shaka tutachukua hatua,” alijibu alipoulizwa ikiwa serikali inapanga kufanya lolote.

 

Baadhi ya taarifa zinasema kuwa mhubiri huyo aliyejitangaza mtume pamoja na mke wake walitoroshwa nchi humo kwa njia haramu na genge la watu ambalo linahusika na uuzaji wa magari yaliyoibwa nchini Afrika Kusini na kupelekwa Malawi.

 

Pia kuna baadhi ya vyombo vya habari vya Afrika Kusini vilivyosema kuwa nabii huyo alitoroka kwa kutumia ndege ya rais. Hata hivyo serikali zote mbili zimekanusha madai hayo.

 

Leave a Comment