
MWANAMKE anayeitwa Gladys anapata matibabu katika hospitali ya Orerokpe iliyopo katika jimbo la Delta , kusini mwa Nigeria, baada ya mume wake kumfungia ndani ya seng’enge kwenye chumba chake kwa muda wa miaka minne.
Harrison Governor, ambaye alikuwa mmoja wa watu waliofichua tukio hili aliliambia shirika la utangazaji la Uingereza (BBC) jinsi mme wake Gladys alivyomfungia kwenye kichumba kidogo kilichopo katika eneo la nyumba yao kwa sababu alimtuhumu kuwa mchawi.
Gladys aliokolewa kutoka kwenye eneo hilo lililofungwa Jumatano, na ilifichuliwa kuwa alikuwa akijisaidia mahali hapo haja ndogo na kubwa na kupewa kipande kimoja cha mkate pekee kama chakula cha siku nzima. Gladys kwa sasa yuko katika hospitali ya Orerokpe Hospital ambako anapokea matibabu.
Harrison anasema Gladys alikuwa na watoto wanane, na watatu walifungwa pamoja naye katika chumba hicho.
“Jina lake ni Gladys, na anatoka katika kabila la Ozoro jimbo la Delta, na anaonekana kuwa na umri wa miaka 40 na zaidi…hayuko katika hali nzuri kwa sababu tangu jana hajaweza kuzungumza lolote.

“Lakini tunataka kumpeleka hospitalini ili afanyiwe vipimo. Mme wake kwa sasa yuko katika kituo cha polisi ,” alisema Harrison na kuongeza kuwa kwa sasa, waziri wa masuala ya wanawake katika jimbo hilo anawatunza watoto wake wa kike kwa sababu bado ni wadogo.
Aliongeza kuwa wakati mama yao akihudumiwa kabla hajapona, wataangalia jinsi ya kufungua kesi kwa idara ya upelelezi wa makosa ya jinai .
Msemaji wa polisi katika jimbo la Delta, Onome Umukoro, aliithibitishia BBC tukio hilo, akisema kuwa mme wake Gladys tayari yuko mikononi mwa polisi na anaendelea kufanyiwa uchunguzi.
Umukoro alieleza kuwa mume wa Gladys alikuwa amewaambia kuwa Gladys ana matatizo ya kiakili na kwamba anashutumiwa kuwa mchawi, ndiyo maana bado alikuwa anaishi nae.
Amesema alijaribu kuwatembelea waganga mbalimbali wa kienyeji ili wamtibu lakini ilishindikana. Pia alisema kuwa alimrudisha katika familia yake lakini walimkataa na wakakataa kumkubali kwahiyo alilazimika kumrudisha nyumbani na kuendelea kuvumilia kuishi nae.