MBUNIFU maarufu wa mitindo hapa nchini, Ally Rehmtullah usiku wa kuamkia leo amezindua onesho lake la mitindo alilolipa jina la Kwetu kwetu.
Rehmtullah ambaye amekuwa akifanya maonesho makubwa kama hayo kila mwaka onesho hilo alilizindulia Hoteli ya Serena iliyopo Posta jijini Dar, ambapo wanamitindo walipita jukwaani na kuonesha mitindo mbalimbali ya ubunifu jukwaani.
Onesho lilihudhuria na umati mkubwa wa wageni waalikwa na wabunifu maarufu wa mitindo kama vile Kadija Mwanamboka, Mustapha Hassanali, Martin Kadinda na wengineo.
Wakati wanamitindo wakipita jukwaani na mitindo mbalimbali ya kuvutia wageni waalikwa walilipuka kwa mayowe ya furaha na kuwashangilia.
Baada ya onesho hilo Rehmtullah aliwashukuru wageni waalikwa wote waliojitokeza kwenye onesho hilo na pia kuwashukuru wadhamini waliojitokeza kumpa sapoti ya uzinduzi huo wakiongozwa na Kampuni ya magari ya Mercedes Benz.






