
KIUNGO mshambuliaji fundi wa Simba Mzambia, Clatous Chama ametaja siri ya mabao yake mawili ya ushindi aliyoyafunga nyota huyo walipocheza dhidi ya Polisi Tanzania.
Mzambia huyo alifunga mabao hayo akitokea benchi akichukua nafasi ya Mghana Bernard Morrison ambaye kuingia kwake kulionekana kubadilisha mchezo na kufanikiwa kuvuna pointi tatu na kufi kisha pointi 26.
Fundi huyo aliwekwa benchi kwa makusudi na kocha wake Mbelgiji Sven Vandenbroeck kwa ajili ya kumpumzisha nyota huyo aliyetumika kwenye michezo iliyopita.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Chama alisema lengo la kuifungia mabao hayo ni kuulinda na kuutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara wanaoutetea kwenye msimu huu.
“Kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kufanikiwa kuamua ushindi wa mabao 2-0 nilioupatia timu yangu nikitokea benchi, kikubwa malengo ya ushindi huo ni kuhakikisha ninautetea ubingwa wa ligi.
“Hivyo, nitahakikisha ninaendeleza rekodi nzuri ya ubingwa nikiwa ndani ya kikosi cha Simba, hiyo ndiyo siri kubwa ya mimi kufunga mabao hayo mawili muhimu yaliyotupa pointi tatu.
“Bado nina kazi ya kufanya nikiwa na timu yangu ya Simba na zaidi ni kuhakikisha ninatengeneza na kufunga mabao kwa kila nafasi nitakayoipata kwani hiyo ni kazi yangu,” alisema Chama
STORI: WILBERT MOLANDI