
Mrembo anayekiwasha kwenye tasnia ya Bongo Fleva, Maua Sama anadaiwa ‘kuwafokea’ kiaina warembo wenzake kwenye fani hiyo, Zuhura Othman ‘Zuchu’ na Faustina Charles ‘Nandy’, IJUMAA limedokezwa.
Kwa mujibu wa watu wa karibu wa Maua, amekuwa akifanya vizuri na kuweka rekodi zake bila kelele kama wanavyofanya Zuchu na Nandy.
Watu hao wameliambia Gazeti la IJUMAA kuwa, Maua amekuwa akiachia nyimbo kali mara kwa mara na kufanya vizuri kutokana na kuwa na sauti maridhawa hiyo kukubalika kwa mashabiki wake.

Uchunguzi wa Gazeti la IJUMAA umebaini kwamba, Maua ni miongoni mwa wasanii kike wa Bongo Fleva ambao wamepenya moja kwa moja na kukubalika kwa mashabiki wao.Kufuatia kuwepo kwa maneno hayo kutoka kwa watu wake wa karibu, IJUMAA limefanya mahojiano maalum na Maua juu ya muziki wake na kama ni kweli hapendi kufanya kiki kama ilivyo kwa akina Zuchu na Nandy;
IJUMAA: Kwanza kabisa Maua ni kama umepotea kidogo, ni kwa nini?
MAUA: Hapana, sijapotea, ila ukweli ni kwamba kwenye muziki wetu ni lazima ifike wakati ujipumzishe kidogo, upate wakati wa kutafakari ni kitu gani ufanye ili mashabiki wakuelewe hivyo ndiyo maana mtu unapumzika kidogo.
IJUMAA: Wengi wanaamini kuwa, ukipumzika kidogo tu kwenye gemu wanaibuka wengine haraka, halafu wewe unazima, hii ikoje?

MAUA: Mwenye kipaji anacho tu na ukweli bila kufanya hivyo unaweza ukapata stresi na mwisho wa siku, ukakata tamaa ya kuendelea na muziki.
IJUMAA: Uliwahi kufikiria kuacha muziki?MAUA: Mara nyingi, lakini mwisho wa siku unakumbuka kuwa una mashabiki wengi tayari na wanakufuatilia hivyo unaamua kukaza buti.
IJUMAA: Je, ni kwa nini wasanii wengi wa Bongo Fleva wanapitia kwenye stresi na wengine kujitumbukiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya?
MAUA: Mtu asikwambie kitu; kazi hii ya muziki ina changamoto sana kwa sababu kila mara unawaza ni jinsi gani utashibisha nyonyo za mashabiki wako, tena kwa upande wetu sisi wanawake, tunapitia mitihani mingi.
Ni kwa vile tu wanatuona kwa nje, wanafikiri hadi ndani tuna amani. Sisi ni watu ambao tunapitia wakati mgumu sana. kama mtu una moyo mwepesi, unaachana kabisa na kuimba.
IJUMAA: Kumeibuka wasanii wa kike kama Zuchu Nandy Lulu Diva na wengine ambao wanafanya vizuri, kwa upande wako umejipangaje ili uendelee kuwepo ulipo?
MAUA: Unajua kila mtu ana uimbaji na mashabiki wake. Kingine kuwepo wanamuziki wengine wa kike ni jambo jema kwa sababu tulikuwa wachache ili tuweze kupata changamoto tusijisahau.
IJUMAA: Wasanii wengi kama hao akina Zuchu na Nandy wanadaiwa kutumia kiki ili kupaisha kazi zao, je, kwa upande wako unalichukuliaje jambo hilo?
MAUA: Mimi siamini katika kiki, lakini kama wao wanaamini hivyo waache, badala yake, kazi zao ziseme zenyewe.Kwa kweli sipendi kiki na ninamuomba Mungu sana aniepushe na hilo maana ninaweza kupinga, halafu ikaja ikanitokea, namuomba Mungu aniepushe na hilo.
IJUMAA: Mara nyingi anaonekana mama yako kwenye video zako nyingi akiimba na kukusapoti, unakuwa umempanga?
MAUA: Mama yangu ni shabiki wangu mkubwa; yaani alianza kunisapoti tangu mara ya kwanza. Unajua msichana ukiingia kwenye muziki inavyokuwa ngumu wazazi kupokea, lakini wazazi wangu walinipokea vizuri sana.
IJUMAA: Umekuwa ni msanii ambaye hupendi kabisa kuweka uhusiano wako wa kimapenzi wazi, ni kwa nini?
MAUA: Niliamua tu, maisha yangu binafsi yawe binafsi na si kwenye mitandao.
IJUMAA: Lakini kuna kipindi ilisemekana unataka kuolewa na mzungu na mpaka akaenda nyumbani kwenu Moshi, je, iliishia wapi?
MAUA: Ndiyo maana nikasema kuwa maisha yangu binafsi kama hayo ninayaficha kidogo, lakini siku ikitimia yatakuwa wazi.
IJUMAA: Unamzungumziaje MwanaFA maana naona upo naye karibu?
MAUA: Ninampenda; yaani yule baba ana roho yake, acheni nimpende, amenitoa mbali.Maua amekimbiza mno na nyimbo kama vile Iokote, Mahaba Niue, Nioneshe, Gusanisha na nyingine kibao na sasa anakiwasha na Wimbo wa Kan Dance.
Stori: Imelda Mtema