
Mfalme wa Uingereza, King Charles III, ameripotiwa kutoa mwaliko kwa mwanawe mdogo, Prince Harry, pamoja na mkewe Meghan Markle na watoto wao wawili, Prince Archie na Princess Lilibet, kukaa katika moja ya makazi ya kifalme wakati wa ziara yao inayotarajiwa kufanyika nchini Uingereza mwezi Julai.
Taarifa hizo zinakuja huku familia ya Sussex ikitarajiwa kutembelea Uingereza kwa pamoja kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2022. Ziara hiyo inahusishwa na shughuli za kuelekea kuhesabu mwaka mmoja kabla ya kuanza kwa michezo ya Invictus Games Birmingham 2027, mashindano yanayowashirikisha wanajeshi na maveterani wenye ulemavu.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Mfalme Charles ametoa ofa ya makazi kwa familia hiyo katika eneo la kifalme, ingawa hadi sasa Prince Harry na Meghan Markle hawajatoa majibu kuhusu mwaliko huo.

Hata hivyo, suala la usalama linaendelea kuwa moja ya changamoto kubwa kwa Duke na Duchess wa Sussex. Tangu walipojiondoa katika majukumu rasmi ya kifalme mwaka 2020, walipoteza ulinzi wa polisi unaofadhiliwa na walipa kodi wa Uingereza, jambo ambalo Prince Harry amekuwa akilipinga kupitia mahakama akidai kuwa familia yake inahitaji usalama wa kutosha wanapokuwa nchini humo.
Prince Harry amekuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa anataka watoto wake waione Uingereza kama nyumbani kwao, lakini amesema hilo haliwezekani bila kuwa na uhakika wa usalama wao wanapokuwa nchini humo.
Ingawa hakuna ratiba rasmi iliyotangazwa kuhusu uwezekano wa kukutana kwa Prince Harry na Mfalme Charles wakati wa ziara hiyo, wawili hao waliwahi kukutana kwa mazungumzo ya faragha mjini London mwezi Septemba mwaka 2025, ikiwa ni mara yao ya kwanza kuonana ana kwa ana baada ya kipindi cha miezi 19.
Prince Harry amekuwa akitembelea Uingereza mara kadhaa tangu alipoondoka kwenye majukumu ya kifalme, lakini Meghan Markle pamoja na watoto wao hawajarejea nchini humo tangu mwaka 2022.