×

Kaze Aleta Beki wa Kazi Yanga

YANGA imeanza kufanyia kazi ripoti ya usajili iliyowasilishwa na kocha mkuu wa timu hiyo, Cedric Kaze, ambapo ipo kwenye hatua za mwisho za kumchukua beki wa kazi, Iddi Mobby anayeitumikia Polisi Tanzania.

 

Tangu Kaze aanze kukinoa kikosi hicho, amekuwa akisisitiza nia yake ya kusajili wachezaji mbadala katika kila safu huku akisisitiza kuwatoa kwa mkopo wengine ambao anaona hawaendani na kasi yake jambo ambalo sasa limeanza kutimizwa.

 

Chanzo chetu kimelieleza Spoti Xtra kwamba, tayari uongozi wa Yanga, umeshaanza kutekeleza zoezi hilo la usajili, ambapo tayari imekaribia kuikamata saini ya beki wa kati wa Polisi Tanzania, Iddi Mobby.“

 

Tuko kwenye mipango ya usajili ambayo inatokana na ripoti ya kocha wetu, hivyo hadi muda huu tayari wachezaji wote ambao kocha amewahitaji, tulishawafuata na kuzungumza nao, kubwa zaidi tunatarajia kuanza kuwatangaza mapema tu kabla ya dirisha la usajili kufungwa,” kilisema chanzo hicho.

 

Spoti Xtra lilimtafuta Mobby ili azungumzie dili lake na Yanga, ambapo alisema: “Ni kweli nilishawasiliana na Yanga, wana nia ya kunisajili ila walisema wataniambia mara tu watakapokuwa tayari wamekamilisha mambo yao maana walisema wana mpango wa kuwatoa baadhi ya nyota wao kwa mkopo ndiyo watarejea kwangu.“

 

Mimi nipo tayari kuichezea Yanga endapo tu wakija kuzungumza na klabu yangu maana bado nina mkataba na Polisi ambao unafi kia ukomo mwisho wa msimu huu.”

STORI: MUSA MATEJA

Leave a Comment