×

JPM Afungua Shule ya Ihungo, Aonya Wanafunzi Kuendelea Kukaa Chini Dar – Video

RAIS John Magufuli, akiwa katika ziara mkoani Kagera, leo Januari, 2021, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha Veta Mkoa wa Kagera na kufungua Shule ya Sekondari ya Ihungo ambayo ilibomolewa na tetemeko la ardhi la Septemba 10, mwaka 2016 kisha kujengwa upya na Serikali.

 

Akizungumza na wananchi wa Bukoba shuleni hapo, Magufuli amewashukuru wananchi wa Kagera kumpa kura nyingi, na kusema aliyowaahidi atayatimiza. Pia amewashukuru kwa kumchagua Mbunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Byabato ambaye amemteua kuwa Naibu Waziri wa Nishati.

Miongoni mwa kauli muhimu alizozitoa Rais Magufuli ni:

“Wana Kagera nawashukuru kwa kunipa kura nyingi sana, nilikuja hapa kuwaomba kura hapa na nikawaombea kura wabunge na madiwani, kwa upendo mkubwa sana mlifanya mabadiliko ya kweli, naahidi yale tuliyoahidi kuyatimiza.

 

“Leo nimeweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha VETA katika Mkoa huu wa Kagera, Serikali ya China ilitusaidia sh. bilioni 22 kwa ajili ya ujenzi wa chuo hiki kikubwa sana na kimeanza kujengwa na tunategemea mwaka huu kitakamilika.

 

“Kuna shule moja ya Msingi ipo Ubungo Dar es Salaam, inaitwa Barango, ina wanafunzi wengi tu na bado wanakaa chini, madarasa mengine yamebomoka, madawati yamevunjika DC, RC, Mkurugenzi na mbunge yupo na ni Profesa wa Elimu, na wanakusanya kodi.  Naongea nikiwa Kagera nikifika Dar, nisikute wanafunzi wanakaa chini, nitakwenda kukagua mwenyewe, ‘message sent and delivered!’

 

“Hii ni dhambi kwangu kwamba nilikosea kuwachagua baadhi ya viongozi, ndiyo maana nilipofika hapa sikutaka madarasa ya kuandaliwa nikawa navamia madarasa nikakuta madawati yapo, nikasema Haleluya hongereni sana, lakini hiyo shule ya Ubungo maneno haya wayasikie.

 

“Namshukuru mwandishi ameitoa kwenye mitandao (taarifa ya wanafunzi wa Barango, Ubungo Jijini Dar es Salaam) kuwa wanafunzi wanakaa chini. Viongozi wa kule wakaanza kusema ni masuala ya kisiasa, hayo sio masuala ya kisiasa, hayo mimi ndiyo napenda kuyajua.

 

“Ninazungumza nikiwa Kagera lakini nikienda Dar es salaam niyakute madarasa ya Shule ya Barango yamekamilika na Wanafunzi hawakai tena chini, nitaenda kuitembelea Mimi hiyo Shule, kama wananisikia meseji sent na imewafikia.

 

“Kuna sehemu watu wanafanya kazi lakini wengine wanalala, ndiyo maana DED wa Geita nilimfukuza kazi, ananunua gari la milioni 400 huku watu wanachangishwa madawati, ananunua mpaka mabasi ya kusafirisha wafanyakazi, viongozi tuzitumie vizuri fedha za wananchi.

 

“Nilipokuja hapa Kagera walitaka hizi hela nizigawe nikanunue ndizi na mahindi, nikasema sitoi kitu, najua nilionekana wa hovyo kwa baadhi ya wanasiasa huwezi ukawagawia watu wote wa Kagera chakula nilitaka kuwaambia ukweli.

 

“Hongereni sana Kagera tuendelee kuzalisha mazao mengi, mvua zinanyesha Corona hatuna na Mungu akatusaidia akasema nataka Corona isiwepo Tanzania ikafutwa moja kwa moja na ndiyo maana hapa hakuna aliyevaa barakoa, tunamshukuru Mungu.

 

“Mabishano kati ya Anatoly na Balozi Kagasheki yameichelewesha Bukoba, hivyo tusirudi huko, leo nimeyasema haya sababu sikuja kuomba kura, kama wamenipigia kura na hawatonipigia tena kura siku nyingine kwa sababu sitegemei kuomba urais.

 

“Kila mara nitapozungumza Tanzania ni matajiri, kweli sisi ni matajiri ndiyo maana tunashirikiana na matajiri wenzetu kama China na Uingereza tunawashukuru sana matajiri wenzetu Uingereza ambao tumeshirikiana nao kuijenga Shule ya Ihungo ambayo iliathiriwa na Tetemeko.

 

“Nimezindua Shule ya Sekondari ya Ihungo ambayo imejengwa na kuwa mpya, shule hii iliathiriwa sana na Tetemeko ila leo ina majengo mazuri kama chuo kikuu, nawashukuru marafiki zetu Uingereza ambao tumesadiana nao kwenye ujenzi wa shule hii, anayekufaa kwa dhiki ndiye rafiki.

 

“Mpaka sasa nchi yetu ina vyuo vya VETA 712, ambapo vimeongezeka kutoka vyuo 672 mwaka 2015, kati ya hivyo vya serikali vipo 62, ambapo 20 ni vya ngazi ya mkoa na 42 ni vya ngazi ya wilaya, 2020 vimedahili wanafunzi 226, 767.

 

“Kesho tutakuwa na utiaji saini wa mradi mkubwa sana utakaofanyika Mkoa wa Kagera, ambapo makampuni ya Marekani, Australia na Uingereza yatashiriki katika uchimbaji wa Kabanga Nickel na Watanzania wengi watapata ajira.

 

Leave a Comment