
KATIBU wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Sengerema, Khatwabu Mohamed, amempongeza Mbunge wa Jimbo la Buchosa, Mhe. Eric Shigongo, kwa kusimamia vizuri na kutekeleza vyema Ilani ya uchaguzi ya CCM na kuongeza kuwa, Shigongo amekuwa mfano kwa wabunge wengine na wao waige mfano huu.
Kauli hiyo ameitoa baada ya Shigongo kuanzisha kampeni yake ya BUCHOSA MPYA, PELEKA MTOTO SHULE ambapo ameanza zoezi la ugawaji wa sare za shule na madaftari kwa wanafunzi ambao wanatoka katima familia zisizo na uwezo ndani ya jimbo hilo ili kuwahimiza wazazi kuwapeleka watoto wao shule, kuwapunguzia sehemu ya gharama watoto na kuchochea kiwango cha elimu kwa watoto jimboni humo.
“Sisi kama chama tunajisikia faraja kuona ndani ya muda mfupi tu tangu Shigongo achaguliwe na kuapishwa, Ilani anaifanyia kazi vizuri, tunamuomba aendelee kutekeleza Ilani hiyo kwa kuwahudumia wananchi na kuwa nao karibu.
Pia, tunawaomba na wabunge wengine waige mfano huu, lakini tunawaomba wananchi wa Jimbo la Buchosa na Sengerema kutoa michango yao na kujitolea katika masuala ya maendeleo ili kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano na viongozi wetu tuliowachagua katika uchaguzi mkuu,” alisema Mohamed.
Mbali na kugawa vifaa hivyo kwa watoto wanaotoka katika familia zisizo na uwezo, Shigongo pia ameendelea kugawa madaftari kwa kila mwanafunzi wa darasa la kwanza katika shule zote za Jimbo la Buchosa. Mpaka sasa, jumla ya wanafunzi 46 wanaotoka kwenye familia zisizo na uwezo wamepatiwa sare za shule pamoja na madaftari, huku akigawa jumla ya madaftari 1,930 kwa wanafunzi wa shule mbalimbali kwenye kata hizo.