
UONGOZI wa Simba umesema kuwa tayari umepata Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ya mshambuliaji wao Mnigeria Junior Lokosa huku wakipanga kuipambania ya kiungo wao mpya mshambuliaji Perfect Chikwende.
Hiyo ikiwa ni siku chache uongozi wa timu hiyo ukamilishe mipango ya usajili wa nyota hao watakaowatumia kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Bara.
Simba imemsajili Chikwende akitokea FC Platinum ya nchini Zimbabwe baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji Sven Vandenbroeck kupendekeza usajili wake katika dirisha dogo.

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Simba, (CEO), Barbara Gonzalez alisema kuwa bado hawajapata ITC ya Chikwende kutokana na kile anachodhani kuwa ni utaratibu wa mtandao wa Zimbabwe.
“Shirikisho la Zimbabwe limekuwa taratibu sana kwenye upande wa kuthibitisha na kujibu kuhusu haya ila nina amini kwamba kati ya siku hizi mbili, tatu inaweza kuwasili.
“Wanasimba waondoe hofu kabisa, ITC yake itakamilika kwa wakati kabla ya kuendelea kwa michuano ya kimataifa na ligi inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.“Kuhusu leseni yake ya kucheza ligi yenyewe tayari tumeipata kutoka TFF, anasubiria kuanza kwa ligi ili aanze kuonyesha makali yake.“
Lokosa yeye tayari tumepokea ITC yake kutoka Chama cha Soka cha Nigeria ambaye usajili wake wa kucheza michuano ya kimataifa pekee,” alisema Barbara.