
WAZIRI wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo, ametangaza kuanzia Februari Mosi hadi 7, 2021, zitakuwa siku saba za kupiga nyungu kwa Watanzania ili kuchukua tahadhari dhidi ya ya ugonjwa wa Covid19.
Akizungumza mkoani Tabora leo Jumamosi Januari 30, 2021, katika ziara ya Rais John Magufuli, waziri huyo amesema wananchi wanatakiwa kuendelea na majukumu ya kujenga taifa bila hofu sambamba na kuchukua tahadhari kwa kupiga nyungu akimaanisha kujifukiza.
“Rais Magufuli juzi ulisema Watanzania tuko salama, angalia umati huu wote tuko salama, hapa corona haina nafasi, tutaendelea kumuomba Mungu na umesema watu wajifukize sana, Jumatatu tunaanza kampeni nyingine ya wiki moja (season three) nyungu kama kawaida,“ alisema Jafo.
“Hapa Corona haina nafasi, tunajifukiza, tunakula matunda, tunamuomba Mungu. Season three, nyungu kama kawaida, tunaanza Februari 01 hadi Februari 07, 2021, hatupoi; kazi inaendelea, uchumi wetu lazima usimame. Hakuna Mtanzania atajifungia ndani kwa ajili ya hofu ya ugonjwa huu, wote tutapiga nyungu, baada ya hapo shughuli nyingine ziendelee kama kawaida,” amesema na kuongeza kwamba hakuna hofu ya kuacha kufanya shughuli za maendeleo na nyungu ni shughuli inayotakiwa kufanyika mara kwa mara.