
MSANII wa muziki kutoka Ghana, Ama Serwah Genfi ‘Amaarae’ amepata shavu baada ya kutangazwa kuwa msanii bora katika mpango wake wa kuendeleza wasanii ujulikanao kama ‘Africa Rising Artist Development Program’.
Mbali na kuwa mwimbaji, Amaarae pia ni mwimbaji anayekuja juu kwa sasa miongoni mwa wasanii wa kike, ukanda wa Afrika.
“Inashangaza kuchaguliwa na Apple Music kuwa msanii wake anayechipukia, yaani Africa Rising Artist. Upendo na uungwaji mkono wa albam husika uliotolewa na familia ya Apple Music, kusema ukweli, umekuwa ni mkubwa mno.
“Hakika nimepewa heshima kubwa na moja kwa moja nalishirikisha kundi langu la Angel Army ambao najua watafurahi kama mimi. Ninatumaini kampeni itakayofuata itakuwa ni ya mafanikio makubwa,” anasema Amaarae.

Amaarae, ambaye amekulia Ghana, Georgia na New Jersey, Marekani, amekuwa na umahiri mkubwa wa tamaduni mbalimbali ambapo utunzi wa muziki wake umechukua sehemu kubwa ya urithi wa nchi za Afrika Magharibi.
Baada ya kushusha albam yake yenye madoido kibao ya Passionfruit Summers (2017), Amaarae aliitumia fursa hiyo kutoa kibao cha ‘Spend Some Time’ kilichomshirikisha Wande Coal na ‘Like It’ ambacho ndicho kiliimarisha zaidi umaarufu wake.
Albam yake yenye nyimbo 14 ya hivi karibuni iitwayo THE ANGEL YOU DON’T KNOW ina vionjo mbalimbali vya muziki wa Afrika, Pop, R&B, ambavyo vilimpa umaarufu mkubwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari hasa vya Marekani.
Mpango huo wa Apple Music wa Africa Rising unanuia kuinua wasanii chipukizi, una lengo la kuendeleza, kutambua na kufichua vipaji mbalimbali ambavyo vitakuwa nyota wa baadaye wa Afrika.
Africa Rising utashuhudia Apple Music ikichagua wasanii sita kila mwaka ambao watapata misaada ya nguvu kupitia kituo cha radio cha Apple Music. Nyota waliopita wa Africa Rising Artistist ni Omah Lay, Manu WorldStar na Tems.
Africa Rising ni moja ya hatua nyingi za Apple Music zilizolenga kuibua vipaji vya Afrika na kuvisambaza duniani.

Ikiwa katika nchi 33 sasa za Kusini mwa Jangwa la Sahara, Apple Music unajumuisha kituo cha Africa Now Radio ambacho kimeendesha mahojiano na wasanii wakali kama Tiwa Savage, Davido, Sho Madjozi, Yemi Alade, Cassper Nyovest, Fireboy DML, Omah Lay, Mr Eazi, Patoranking, Rayvanny, Adekunle Gold na Master KG.
Aidha, imemchagua mwanamuziki nyota wa Nigeria, Rema, kuwa mmoja wa nyota watakaofuata, baada ya Burna Boy kuongezwa katika orodha ya mwaka 2019 na Mr Eazi aliyechaguliwa mwaka 2017.
Mwandishi Wetu.