×

Beki Mpya Simba ni Kocha Mchezaji

KAMA Kocha Mkuu wa Simba, raia wa Ufaransa, Didier Gomes Da Rosa atamtumia beki wake mpya raia wa Zimbabwe, Peter Muduhwa ni wazi kuwa anaweza kuwa na faida katika michezo ya timu hiyo inayofuata.

 

 

Beki huyo alionyesha uwezo wa juu katika mazoezi ya mwisho kabla ya Simba kusafiri kwenda DR Congo kwa ajili ya mchezo dhidi ya AS Vita Club utakaochezwa leo, alimfurahisha kocha wake mkuu, Gomes Da Rosa na wachezaji wenzake kiasi cha kumpigia saluti.

 

 

Muduhwa ambaye alikuwa anaichezea Highlanders FC ya nchini Zimbabwe, alijiunga na Simba hivi karibuni akitokea nchini Cameroon alikokuwa akishiriki kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Zimbabwe katika michuano ya CHAN, alikuwa akifanya mazoezi huku akionekana kama ni mwalimu kwa wenzake ndani ya uwanja kwa jinsi alivyokuwa akiwaelekeza.

 

 

Chanzo cha uhakika kutoka katika benchi la ufundi la Simba kimeeleza kuwa Gomes amepata matumaini makubwa ya kumtumia mlinzi huyo, maana yupo fiti huku safu ya ulinzi hasa wa kati ikitajwa kuwa na tatizo pindi inapocheza kimataifa.

 

 

“Nina imani kubwa ya kumuona Muduhwa akichezeshwa katika mchezo wetu na AS Vita, maana kocha amefurahishwa na utimamu wa mwili wake, kiasi kwamba hata wachezaji wenzake wamejikuta wakimfurahia kutokana na uwezo wa kukaba na kuwapanga wenzake muda wote wa mchezo jambo ambalo lilikuwa likitimizwa na Pascal Wawa pekee.

 

 

“Kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Simba B, Muduhwa alicheza muda wote na kwamba alionekana kuitawala safu hiyo jambo lililomfanya kocha na wachezaji wenzake wampigie saluti, huku kocha akionyesha kufurahi zaidi,” kilisema chanzo hicho ambacho kiliongeza kuwa inawezekana huyo akawa mrithi sahihi wa Wawa ambaye umri umeanza kumtupa mkono.

Leave a Comment