
WACHEZAJI wawili wa kikosi cha Yanga, Said Ntibanzokiza ‘Saido’ na Yacouba Sogne, pacha yao inaonekana kuendelea kutusua hata chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Juma Mwambusi.
Nyota hao wawili wamehusika kwenye jumla ya mabao 16 kati ya mabao 37 yaliyofungwa na kikosi hicho ambacho kimecheza jumla ya mechi 24, sawa na dakika 2,160.
Yacouba amehusika kwenye jumla ya mabao 9 akiwa amefunga mabao matano huku akitengeneza jumla ya nafasi nne zilizoleta mabao katika kikosi hicho kinachoongoza ligi na pointi zake 51.

Kwa upande wa Saido amehusika kwenye mabao 7 akiwa ametupia mabao matatu na kutengeneza pasi nne za mabao katika kikosi hicho kwa msimu wa 2020/21.
Mwambusi ameliambia Championi Jumatatu kuwa ana kazi ya kutengeneza pacha ambazo zitakuwa zinampa matokeo kwenye mechi zake kwa kuwa ushindani kwenye ligi ni mkubwa.
Kwenye mchezo wake wa kwanza baada ya kurejea kwenye benchi la ufundi kutokana na kufutwa kazi kwa Cedric Kaze, Machi 7, mchezo wake wa kwanza mbele ya KMC alishuhudia pacha hizo mbili zikimpa pointi moja baada ya Saido kutengeneza nafasi ya bao lililofungwa na Yacouba wakati ubao ukisoma Yanga 1-1 KMC.
STORI NA LUNYAMADZO MLYUKA, Dar es Salaam