
MSIMU wa pili wa utoaji wa tuzo za kuwapongeza wanawake viongozi barani Afrika zijulikanazo kama ‘WIMA Awards’ zinatarajiwa kufanyika leo Jumamosi Mtana Hall LAPF Tower jijini Dar es Salaam.
Tuzo hizi zilianzishwa rasmi mwaka 2019 kwa lengo la kuwatambua zaidi na kuwapongeza wanawake wanaofanya vizuri katika nafasi mbalimbali za uongozi barani Afrika.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Mkurugenzi Mkuu wa CV People of Tanzania, Naike Moshi alisema kuwa tuzo hizo za mwaka 2021 zitafanyika rasmi leo baada ya kusogezwa mbele ili kupisha maombolezo ya msiba wa Hayati John Pombe Magufuli.
Naike alisema kuwa, mwaka huu wameongeza vipengele vingine saba ikiwemo SDG female champion, WIMA Stem Awards, Next Gem WIMA Awards, ‘He for She’ Leadership Award, WIMA abilities Award, WIMA Lifetime Award and Exemplary Female Leadership during Covid-19 crisis.
Alisema kuwa tuzo hizo ni za wazi na kila kipengele wamepatikana washiriki baada ya kuchaguliwa na kupigiwa kura na umma, zoezi lililofanyika kwa miezi miwili na washindi watatangazwa rasmi leo.
“Nina imani kubwa kuwa tuzo za WIMA zitabaki kuwa tuzo kubwa zaidi barani Afrika katika kuwahamasisha na kuwatambua wanawake wanaofanya vizuri katika nafasi mbalimbali za uongozi,” alisema Naike.
Naye mwakilishi kutoka UN Global Compact Network Tanzania, Marsha Yambi alisema kuwa: “Tunayo furaha kuwa sehemu ya tuzo hizi za wanawake viongozi za WIMA.
Ni wazi kuwa tuzo hizi zimefungua milango mingi kwa wanawake na mashirika mbalimbali kupata nguvu kazi inayoleta matokeo chanya kwa uchumi wa nchi.
“Hivyo, sisi UN Global Compact tumeona kuwa tuna jukumu kubwa kuhakikisha kuwa tunashirikiana na taasisi mbalimbali zilizopo nje na ndani ya Tanzania kama CV of People of Tanzania kuhakikisha kuwa tunaleta mapinduzi chanya katika boresha usawa wa kijinsia hususani katika maeneo ya kazi.”