
IMEFAHAMIKA kuwa Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Frederick Mwakalebela, juzi Jumatatu aliwasilisha barua ya kukata rufaa kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).Mwakalebela alifungiwa na Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania kujihusisha na soka ndani na nje ya nchi na kutakiwa kulipa faini ya shilingi milioni 5 kwa kosa la kuitisha Mkutano wa Waandishi wa Habari.
Kosa lingine alilokutwa nalo ni la kutoa maneno ya uchochezi kwa mashabiki na wanachama wa Yanga dhidi ya vyombo vinavyosimamia soka kuhusiana na usajili wa kiungo mshambuliaji wa Simba, Mghana Bernard Morrison.
Championi Jumamosi, lina ushahidi juu ya rufaa hiyo iliyokatwa ya Mwakalebela kutoka kwa mmoja wa viongozi wakubwa wa shirikisho hilo.
“Mwakalebela amekata rufaa kwa siri kubwa baada ya kuwasilisha barua hiyo kwenye shirikisho hilo akipinga maamuzi ya adhabu yake.“
Maamuzi ya rufaa kukatwa yamekuja baada ya Kamati ya Utendaji ya Yanga kukubaliana kwa pamoja kupinga maamuzi ya adhabu hiyo kubwa iliyotolewa na kamati hiyo ya TFF.
“Hivyo muda wowote Mwakalebela ataitwa kwenye kamati hiyo kwa ajili ya kusikilizwa kesi upya, kesi yake hiyo inayomkabili akiwa tayari ameanza kutumikia adhabu yake,” alisema mtoa taarifa huyo.Alipotafutwa Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli kuzungumzia hilo alisema: “Bado sijazipata taarifa hizo, lakini uongozi ulikuwa kwenye mpango wa kuwasilisha rufaa yake.”
WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam