
SERIKALI imesema ipo tayari kupokea mapendekezo ya mabadiliko ya sheria na sera ya vyombo vya habari na kuzifanyia marekebisho kwa maslahi ya sekta hiyo.
Hayo yamesemwa jana na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbasi, katika Kongamano lililoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshugulikia Elimu na Sayansi (Unesco) kwa kushirikiana na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) ikiwa ni sehemu ya maazimisho ya siku ya Uhuru wa Habari Duniani itakayofanyika kitaifa mkoani Arusha, Mei 3.
“Tunakaribisha michango mbalimbali kutoka kwa wadau wa sekta ya habari nchini juu ya mabadiliko ya sera na sheria katika sekta hii, tuleteeni zote ambazo mnadhani zitaboresha sekta ya habari, tupo tayari kupokea na kuzifanyia kazi,” alisema Dk Abbasi.
Kwa upande wa Mwakilishi UNECSO, Tirso Dos Santos, alimesema vyombo vya habari duniani bado vina changamoto nyingi ikiwemo usalama wa waandishi pindi wanapotekeleza majukumu yao, suala alilosema kuwa ni muhimu likazingatiwa.
Alisema vyombo vya habari vina umuhimu mkubwa katika ustawi wa taifa lolote duniani, na kuiomba Serikali na wadau wengine kuvipa ushirikiano wa kutosha ili viweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu.