×

Huzuni- Pacha Wafa Baharini Wakiwa Wamekumbatiana

FAMILIA katika eneo la Gasi, Kaunti ya Kwale nchini Kenya imeghubikwa na simanzi baada ya watoto wao pacha kupatikana wamefariki baharini.

Miili ya wawili hao, Kennedy Gichui na Solomon Macharia wenye umri wa miaka 18, ilipatikana Jumanne Juni mosi mwaka huu wakiwa wameshikana mikono.

Binamu yao, Kennedy Kamau, 16, ambaye alienda nao baharini Jumatatu jioni alifanikiwa kuogelea hadi akakwama kwenye mikoko, akaokolewa na wavuvi.

Alipookolewa ndipo akasema kuna wenzake wawili ambao alikuwa nao baharini. Alikimbizwa hadi Hospitali ya Kinondo kwa matibabu.

Akithibitisha kisa hicho, Mkuu wa Polisi wa Msambweni, Bw Fanuel Nasio alisema miili yao ilipelekwa kuhifadhiwa katika mochari ya Hospitali ya Kwale.

Baba yao, Bw Samuel Njuguna ambaye ni fundi mwashi mashuhuri Msambweni, alisema wavulana hao walikuwa wamehitimu masomo ya Kidato cha Nne, mmoja alipata gredi ya C na mwingine C+.

“Walikuwa wanasubiri kujiunga na vyuo vikuu,” alisema Bw Njuguna.

Bi Clara Kanga, afisa wa uokoaji katika Kaunti ya Kwale ambaye aliongoza oparesheni ya uokoaji, alisema kisa hicho kilitokea mwendo wa saa kumi na moja jioni siku ya Jumatatu.

Bi Kanga alisema wasingefanikiwa kuwatafuta Jumatatu jioni kwa sababu ya giza lilipoingia ndipo wakalazimika kusubiri hadi Jumanne asubuhi.

Baada ya oparesheni iliyofanywa kwa saa mbili ikijumuisha wapigambizi, wavuvi na wenyeji, pacha hao walipatikana karibu na mikoko muda wa saa nne asubuhi.

“Walikuwa wameshikana mikono kumaanisha walikuwa wanajaribu kujiokoa. Mwili mmoja ulikuwa umeelea na mwingine ulikuwa bado umezama,” akaeleza.

Wanakijiji walisema watoto hao walienda kuogelea bila kujua kwamba maji huongezeka sana baharini hasa ifikapo jioni.

“Kuna sehemu ya bahari ambapo ni ghuba. Kwa vile wao ni wageni eneo hili, inawezekana waliendelea kuogelea bila kujua ghuba ingejaa maji,” akasema.

Msimamizi wa Kaunti Ndogo ya Msambweni, Bi Mwanakombo Kilalo, alisema kaunti ilikuwa imetoa ilani kwa wageni kuhakikisha wanaandamana na wenyeji ili wawe salama wanapoenda kuogelea au kutembea ufuoni.
“Nadhani waliona hapakuwa na maji baharini na hawakujua yangeongezeka ghafla,” akasema.

Cc; mushigabriel

Leave a Comment