
Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) amewafutia mashtaka na kuwaachia huru washtakiwa 14 waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka 41 yakiwemo ya kufanya biashara haramu ya kusafirisha binadamu, kukwepa kodi na kuisababishia hasara ya Sh31 milioni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Watuhumiwa hao wameachiwa baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) kuwasilisha hati mahakamani akieleza kuwa hana nia ya kuendelea na shauri hilo.
Walidaiwa kusafirisha walemavu 37 wakiwemo watoto wadogo wenye umri wa miaka saba na 11 kutoka Mikoa ya Tabora, Shinyanga na kuwaleta Dar es Salaam na kuwafanya kuwa ombaomba mitaani kwa lengo la kujiingizia kipato.
Uamuzi wa kuwafutia kesi na kuwaachia huru umetolewa leo Jumanne Juni 22, 2021 na hakimu mkazi mwandamizi, Kassian Matembele wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Awali, wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon amedai kuwa DPP ameieleza mahakama kuwa hana nia ya kuendelea na shauri hilo.
Wakili huyo amedai washtakiwa hao wamefutiwa mashtaka chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ( CPA) sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.
Baada ya upande mashtaka kueleza hiyo, hakimu alikubaliana na ombi hilo na kuwafutia mashtaka na kisha kuwaachia huru.