
Mahakama Kuu imebatilisha hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya kesi ya Jinai iliyokuwa ikimkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake 7.
Mahakama hiyo imeamuru warejeshewe fedha walizolipa kama faini, kiasi cha shilingi milioni 350.
Uamuzi huo umetolewa leo na Jaji Irvin Mgeta.
Akisoma mashitaka hayo, Februari 22, 2018, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Faraja Nchimbi alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri kuwa, washitakiwa kwa pamoja walitenda makosa Februari 16, 2018 maeneo ya Viwanja vya Buibui na Barabara ya Kawawa, Mkwajuni wilayani Kinondoni, Dar.
Katika shitaka la kwanza la kula njama; kwa pamoja ilidaiwa Februari Mosi na 16, 2018, Dar, walikula njama pamoja na wenzao ambao hawakuwepo mahakamani ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali; mkusanyiko wenye ghasia na kukiuka tamko kutawanyika.
Ilidaiwa kuwa Februari 16, 2018 katika ya Viwanja vya Buibui na Mwananyamala Kinondoni, washtakiwa hao, wakiwa wamekusanyika na azma ya pamoja waliitekeleza, walifanya mkusanyiko usio halali na kusababisha watu waogope na kusababisha uvunjïfu wa amani.
Katika shtaka la tatu; washtakiwa hao walidaiwa kuwa Februari 16, 2018 katika Viwanja vya Buibui, Mwananyamala na Barabara ya Kawawa-Kinondoni, kwa pamoja na wenzao 12 ambao hawakuwepo mahakamani, walitekeleza mkusanyiko au maandamano yasiyo halali wakiwa na lengo la kuvamia ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na kuleta hofu ya uvunjifu wa amani.
Nchimbi alidai kuwa, Februari 16, 2018 katika Barabara ya Kawawa-Kinondoni, Mkwajuni, washtakiwa hao wakiwa na wenzao 12 ambao hawakuwepo mahakamani walikiuka tamko la kuwataka kutawanyika la Ofisa wa Polisi, Gerald Ngiichi kwa kugoma kutawanyika na kusababisha uvunjifu wa amani ambao ulisababisha hofu na hatimaye kifo cha Akwilina Akwilin na majeruhi kwa askari wawili ambao ni H.7856 PC Fikiri na E.6976 CPL Rahim Msangi.
Katika shtaka la tano lililokuwa linamkabili Mbowe ambalo ni la kuhamasisha chuki; ilidaiwa kuwa, Februari 16, 2018 katika Viwanja vya Buibui wilayani Kinondoni, Dar, Mbowe wakati akihutubia wananchi wa jimbo hilo, alihamasisha chuki isivyo halali kwa kutoa matamshi yafuatayo;
‘Ninapozungumza hapa kiongozi wetu wa Kata ya Kinondoni-Hananasif yupo mochwari…amekamatwa na makada wa CCM kwa msaada wa vyombo vya ulinzi na usalama…wamemnyonga wamemuua.
Halafu sisi tunaona ni jambo la kawaida…tunacheka na Polisi…tunacheka na CCM’.
Nchimbi alidai kuwa maneno hayo, yalikuwa na lengo la kuamsha hisia za chuki miongoni mwa Watanzania.
Katika shtaka la sita, Mbowe alidaiwa kuwa Februari 16, 2018 katika mkutano wa umma uliofanyika Viwanja vya Buibui wilayani Kinondoni, Dar, Mbowe alitamka maneno yafuatayo;
‘Tumejipa kibali cha kutangulia mbele ya haki…haiwezekani wanaume wazima na akili zetu na wake zetu na watoto wetu tukafanywa ndondocha..hiii ni nchi ya ajabu. Mimi leo nipo hapa kulinda taifa…kule Afrika Kusini, Jacob Zuma amelazimishwa kujiuzulu…Robert Mugabe wa Zimbabwe kang’olewa, kang’olewa Waziri Mkuu wa Ethiopia…juzi ameondoka kwa People’s Power. Magufuli ni mwepesi kama karatasi’.
Nchimbi alidai kuwa maneno hayo, yalikuwa ya kuinua hali ya kutoridhika miongoni mwa Watanzania dhidi ya Serikali halali iliyopo. Naye Halima Mdee alidaiwa kuwa Februari 16, 2018 akiwahutubia wakazi wa Kinondoni alitamka; ‘Sihitaji kuwasimulia mandhila yanayomkumba kila mmoja wetu kutokana na utawala wa awamu ya tano… Tunaomba kesho tukamchinje Magufuli na vibaraka wake wote…kama mbwai na iwe mbwai’.
Nchimbi alidai kuwa maneno hayo, yalikuwa na lengo kuhamasisha hisia za chuki miongoni mwa Watanzania.
Katika shtaka la nane la kuhamasisha hali ya kutoridhika, John Heche alidaiwa kuwa, Februari 16, 2018 katika Viwanja vya Buibui alitamka kuwa; ‘Kesho patachimbika, upumbavu ambao unafanywa kwenye nchi hii…wizi unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano…watu wanapotea…watu wanauawa, wanaokotwa kwenye mitaro, lazima ukome’.
Nchimbi alidai kuwa maneno hayo, yalikuwa na lengo la kuamsha hali ya kutoridhika miongoni mwa Watanzania dhidi ya utawala uliopo madarakani.
Katika shtaka la tisa la uchochezi wa uasi, lililomkabili Mbowe, alidaiwa kuwa Februari 16, 2018 katika maeneo hayo, alihutubia mkutano wa hadhara na kutamka kuwa; ‘Ninaongoza mapambano nchi hii kwa sababu tumechoka kuuawa…matokeo ya Watanzania mia watakaokufa wataleta haki katika Taifa hili. Wangapi wapo tayari kuchukua bei hiyo?’
Nchimbi alidai kuwa maneno hayo, yalikuwa na nia ya kuleta chuki na hali ya manung’uniko miongoni mwa jamii dhidi ya utawala uliokuwa madarakani.
Katika shtaka la 10 la uchochezi wa uasi, linalomkabili tena Mbowe alidaiwa kuwa Februari 16, 2018 katika maeneo hayo mkoani Dar, Mbowe alitoa matamshi ya kupandikiza chuki na dharau kwa upande wa raia wa Tanzania dhidi ya mamlaka halali kuwa;
‘Hii nchi inadharaulika…imejengewa misingi wa uwoga, kwa lugha nyingine wanaume ni kama mademu, si unawaona hao wanavaa suruali, waoga, bure kabisa…juzi ametekwa kijana wetu wanasema yupo mochwari, haki ya Mungu ingekuwa nchi nyingine Kinondoni ingekuwa majivu…
Lissu amepigwa risasi machine-gun na vyombo vya dola…Watanzania mnarudi nyuma…kuna mwandishi wa habari leo ana siku 86 amebebwa na vyombo vya dola… suluhu ya nchi hii haipo bungeni. Suluhu ya nchi hii ipo kwa wananchi wenyewe…
lakini ili tupate suluhu hiyo, ni lazima tukubali kubeba majeneza…Inawezekana leo mnaogopa kufa…ni bora tuwabebe wachache hata wakiwa 200 waliokufa katika ukombozi ili hatimaye nchi hii isimame kama nchi ya wanaume wengine katika dunia hii’.
Mbowe pia alidaiwa kuwa alishawishi wakazi wa Kinondoni, kutenda kosa la kufanya maandamano na mkusanyiko usio halali.
Katika shtaka la 12 la kushawishi utendaji wa kosa la jinai, linalomkabili mshtakiwa wa pili Msigwa, katika maeneo hayohayo, Msigwa alidaiwa kushawishi raia na wakazi wa eneo hilo, kutenda kosa la jinai, kwa kutembea mbele ya umma wakiwa na silaha.
Shtaka la 13 ambalo lilimkabili mshtakiwa, Ester Bulaya alidaiwa kuwa Februari 16, mwaka huu katika Viwanja vya Buibui wilayani Kinondoni, Dar alitenda kosa la kukaidi amri halali ya tamko.
HUKUMU
Mahakama iliwakuta na hatia washtakiwa kwenye mashtaka 12 kati ya 13.
Hakimu Simba alisema maneno hayo yaliyotamkwa na Mbowe kwenye kampeni ni ya uchochezi.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwatia hatiani washtakiwa wote katika mashtaka 12, isipokuwa shtaka la kwanza ambalo ni kula njama ambalo limefutwa na Mahakama.
April 8, 2020 baada ya kuwatia hatiani washtakiwa kwa makosa 12, Mahakama ilitoa adhabu kama ifuatavyo;
Hakimu: Madai ya kesi ya Akwilina hapa haipo. Isipokuwa maelezo yaliyopo hapa ni kwamba hali ile ilisababisha kuuawa kwa mtu anayeitwa Akwilina Akwilin. Siwezi kusema Akwilina alikufa maana sina ripoti ya daktari inayothibitisha hilo. Suala la Akwilina siwezi kulizungumzia na siligusii kabisa.
Shtaka la 2: Mahakama iliamuru washtakiwa kulipa faini ya shilingi milioni 10 au kwenda gerezani miezi mitano.
Shtaka la 3: Mahakama iliamuru washtakiwa kulipa faini ya shilingi milioni 10.
Shtaka la 4: Mahakama iliamuru washtakiwa kulipa faini ya shilingi milioni 10.
Shtaka la 5: Mahakama iliamuru Freeman Mbowe kulipa faini ya shilingi milioni 10.
Shtaka la 6: Mahakama iliamuru Freeman Mbowe kulipa faini ya shilingi million 10.
Shtaka la 7: Mahakama iliamuru Halima Mdee kulipa faini ya shilingi milioni 10.
Shtaka la 8: Mahakama iliamuru John Heche kulipa faini ya shilingi millioni 10.
Shtaka la 9: Mahakama iliamuru Freeman Mbowe kulipa faini ya shilingi milioni 5.
Shtaka la 10: Mahakama iliamuru Freeman Mbowe kulipa faini ya shilingi milioni 5.
Shtaka la 11: Mahakama iliamuru Freeman Mbowe kulipa faini ya shilingi milioni 10
Shtaka la 12: Mahakama iliamuru Peter Msigwa kulipa faini ya shilingi milioni 10.
Shtaka la 13: Mahakama iliamuru Ester Bulaya kulipa faini ya shililingi milioni 10.
Mahakama ilisema endapo washtakiwa wakishindwa kulipa faini, wataenda gerezani kwa miezi mitano kwa kila kosa. Wote Walilipa faini zilizotokana na michango ya wananchi na sasa zimeamriwa kurejeshwa.
Stori na Na Sifael Paul | GPL