

Katika kuelekea kufanyika uchaguzi Mkuu wa BARAZA la Taifa la Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), unaotarajiwa kufanyika Julai 8 mwaka huu, Kamati maalum ya kitaifa inayoratibu na kusimamia uchaguzi huo imetoa wito kwa makundi mbalimbali hususani wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kujitokeza kushiriki katika uchaguzi huo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Uchaguzi huo Wakili msomi Flaviana Charles, amesema kuwa uchaguzi huo umeitishwa mara baada ya kuundwa kwa kamati hiyo yenye watu 10 kutoka katika mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), ya kitaifa na kimataifa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, ili kusimamia mchakato huo.
Ameongeza kuwa fomu za kuomba kugombea katika nafasi mbalimbali zitaanza kuchukuliwa rasmi Juni 21 katika Ofisi zote za Afisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya zote 139 nchini na mwisho wa kurudisha fomu hizo ni Juni 24 mwaka huu.
Aidha Mwenyekiti huyo wa kamati ameongeza kuwa ifikapo Juni 25,kutafanyika zoezi la kuchakata fomu zote za wagombea katika Ofisi hizo na kazi hiyo itafanywa na kamati hiyo.
“Ifikapo Juni 26,2021uchaguzi katika ngazi za wilaya utaanza huku Juni 28 uchaguzi wa wajumbe wa Baraza katika ngazi ya mkoa ambapo Julai 5 hadi 8,2021 utakuwa ni uchaguzi wa viongozi wa kitaifa wa baraza, kamati ndogo na wajumbe wa bodi ya uratibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali,”amesema.
Amesema kuwa mnamo Julai 9 hadi 10 kutakuwa na uapisho na makabidhiano ya nyaraka na Ofisi na kuanza kazi kwa watumishi hao.
Wakili Flaviana amewalihimiza watu wote wenye sifa za kugombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi huo kujitokeza kugombea nafasi hizo kwa kuzingatia usawa wa kijinsia na makundi maalum yakiwemo ya watu wenye ulemavu.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Foundation for Civil Society, (FCS) Francis Kiwanga amesema kuwa Baraza hilo ni muhimu katika Taasisi hususani katika kazi zote hizo za kusimamia masuala ya uchaguzi.
“Rai yeti sisi kwa Asasi zote za Kiraia kila mtu aweze kushiriki na watu wachukue fomu na kugombea nafasi hizi zilizotangazwa ,”amesema na kuongeza.
“Ushiriki wa wanawake katika uchaguzi huu ni muhimu sana hivyo tunatoa Rai yetu watu wajitokeze ili baraza liwe shirikishi zaidi na wadau wenye upana,”amesema Kiwanga.