
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeahirisha kutoa hukumu ya kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), David Mattaka na wenzake wawili.
Washitakiwa hao wanaokabiliwa na mashitaka ya kughushi, matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 71.
Mahakama hiyo ilipanga kutoa hukumu jana lakini Hakimu Mkazi Mwandamizi, Janeth Mtega alisema mahakama kuwa hukumu ilikuwa haijakamilika na akaahirisha kesi hadi Agosti 20 mwaka huu.
Wakili wa serikali Joseph Kiula alieleza mahakamani kesi hiyo ilipelekwa kwa ajili ya hukumu na upande mashitaka ulikuwa tayari kwa hukumu.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dk Ramadhan Mlinga na aliyekuwa mwanasheria wa mamlaka hiyo, Bertha Soka.
Mattaka na wenzake wanakabiliwa na mashitaka sita likiwemo la matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 71. Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi zaidi ya 20 na vielelezo.
Ilidaiwa mahakamani kuwa, Oktoba 9 mwaka 2007 wakati Mattaka akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, alitumia madaraka vibaya kwa kusaini mkataba wa kukodisha ndege aina ya Airbus na kwamba mkataba huo unadaiwa kuisababishia serikali hasara ya zaidi.
Katika shitaka lingine Dk Mlinga na Soka walidaiwa kuwa Machi 19, 2008 katika ofisi za PPRA Ilala, Dar es Salaam walighushi muhtasari wa kikao wa tarehe hiyo, wakionesha kwamba mamlaka hiyo ilikaa kikao na kujadili maombi ya kuidhinisha ATCL ikodishe ndege hiyo.