
Mahakama ya Hakimu Mkazi wilaya ya Bukoba mkoani Kagera imemhukumu Mchungaji Merchades Mugishagwe na mkewe Agripina Maganja kutumikia kifungo cha miezi 18 gerezani na kulipa faini shilingi milioni 3, baada ya kumtia hatiani kwa makosa matatu ambayo ni kushindwa kutekeleza wajibu wake kama mzazi, kushindwa kupeleka watoto shule na kujihusisha na vikundi visivyotakiwa kijamii.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 35 ya mwaka 2021 ilifunguliwa February 2, mwaka huu, Mugishagwe na mkewe walikuwa wakituhumiwa kukataa kuwapeleka watoto wao shule kwa madai ya kuwa kufanya hivyo ni dhambi kwa maana maandiko ya Mungu hayaruhusu watoto kwenda shule.
Ushahidi wa kesi hiyo, mchungaji Merchades na mkewe mahakamani hapo, walisema shahidi yao namba tatu ni Mungu, ambaye hakufika mahakamani hapo hivyo ushahidi ukafungwa August 12, 2021 na hukumu yake kutolewa leo Agosti 27, 2021.
Familia hiyo inao watoto watano na wote walikuwa hawasomi na mkubwa kati yao ni wa kike mwenye umri wa miaka 13, mbali na kutokwenda shule, wakiwa wadogo hawajawahi kupelekwa kliniki na pia wakiumwa hawapelekwi hospitali.
Mkuu wa wilaya ya Bukoba Deodatus Kinawiro, alimwagiza afisa elimu ya msingi wa manispaa hiyo, kuwakamata na kuwapeleka shuleni kwa nguvu watoto watatu wa familia hiyo huku wazazi wao wakishtakiwa.
Mchungaji Buberwa wa Kanisa la Wakristo washikao amri za Mungu, ambalo makao yake makuu yako mbinguni, alisema hayuko tayari kuruhusu watoto wake kutenda dhambi kwa kwenda shule, huku mkewe Agripina Maganja, akimweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa Mungu atasimama kuwatetea.