
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inaandaa kitini ambacho kitatoa mwongozo wa jinsi mashirika yasiyo ya kiserikali yatakavyonufaika na misamaha ya kodi iliyopo kwa mujibu wa sheria.
Rais Samia ameyasema hayo leo Septemba 30, 2021 jijini Dodoma wakati wa mkutano mkuu wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (Nacongo) uliozikutanisha NGO zote zinazofanya kazi hapa nchini.
Kauli hiyo ya Rais Samia imetokana na maombi yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Nacongo, DkTt+ Lilian Badi wakati akiwasilisha risala yao kwa Rais Samia kwa kueleza changamoto mbalimbali zinazoyakabili mashirika yasiyo ya serikali.
Ameongeza kuwa changamoto hizo kuwa ni pamoja na kupatikanaji wa misamaha ya kodi kwa mashirika yasiyo ya serikali na changamoto ya upatikanaji na uhuishaji wa vibali vya ukazi kwa raia wasio Watanzania.
“Changamoto hizi zikifanyiwa kazi zitasaidia mashirika yasiyo ya kiserikali kuweza kuchangia maendeleo kwa taifa kwa kushirikiana na serikali,” amesema Dk Badi ambaye alichaguliwa Julai mwaka huu kuwa mwenyekiti wa Nacongo.