×

Mkude Ajiondoa Taifa Stars

MENEJA wa Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ Nadir Haroub ‘Cannavaro’, amefunguka kuwa kiungo Jonas Mkude hatakuwepo katika kikosi cha timu hiyo kutokana na sababu zake binafsi.

 

Kiungo huyo hakuonekana katika mazoezi ya Taifa Stars ambayo yalianza juzi Jumatatu katika Uwanja wa Mkapa mkoani Dar kwa ajili ya maandalizi ya mechi dhidi ya Benin ya kuwania kufuzu kucheza Kombe la Dunia, kesho Alhamisi uwanjani hapo.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Cannavaro alisema kuwa, Mkude hatakuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa katika mechi dhidi ya Benin kwa sababu ameomba yeye mwenyewe kujitoa kutokana na sababu zake binafsi.

 

“Mazoezi yanaendelea vizuri na wachezaji wote wapo salama kabisa kwa ajili ya kuwakabili wapinzani wetu isipokuwa Mkude ambaye ameomba mwenyewe kujiondoa kikosini kwa sababu zake binafsi na hatukuweza kuwa na pingamizi na jambo hilo.

 

“Kwa upande wa maandalizi, yanaendelea kama kawaida, tutakuwa na programu moja ya mazoezi kila siku kwa sababu wachezaji wengi wapo vizuri, hivyo tunatarajia ushindi kuwa katika upande wetu,” alisema meneja huyo.

 

MASTAA WATATU WACHOMOLEWA

Wakati huohuo, mastaa watatu wa kikosi hicho, Bakari Mwamnyeto, Erasto Nyoni na Shomary Kapombe wataukosa mchezo huo kutokana na kutokuwa fiti.

 

Canavaro alisema: “Ni kweli wachezaji wote walioitwa timu ya taifa walifika kambini ila Mwamnyeto na Erasto Nyoni ni majeruhi na walikuja kuripoti na mwalimu akawaruhusu warudi nyumbani, nafasi zao zimechukuliwa na Kibwana Shomari na Kibu Denis.”

Hawa Aboubakhari na Careen Oscar, Dar es Salaam

Leave a Comment