
ALIYEKUWA Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad amesema hapendi kuitwa mstaafu na neno hilo linamchukiza, akidai kuwa taratibu za kumwondoa hazikufuatwa.
Prof. Assad ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati wa mdahalo juu ya kitabu cha Rai ya Jenerali kinachozungumzia umuhimu wa Katiba Mpya.
“Sipendi kuitwa CAG niliyemaliza muda wangu kwakuwa nilitolewa Ofisini kinyume cha Katiba. Jambo hili linaniudhi sana kwakuwa hatukusimamia Katiba vizuri.
“Sijawahi kuona nchi yoyote ile ambayo katiba yake inajilinda yenyewe. Kazi ya kuhakikisha katiba inalindwa naweza kusema inafanywa kiasi kikubwa na mahakama. Katika nchi nyingine Mahakama ndio mlinzi mkuu wa katiba mfano wake ni Marekani.
“Kwa mfumo wa Tanzania unaweza kuona dola na Bunge viko karibu sana, mtu anakuwa Mbunge akiteuliwa kuwa Waziri au Naibu Waziri anarudi tena kwenye dola huku akiwa bado ni sehemu ya Bunge.
“Kwa rai yangu mimi tutafute majaji makini na tukishawapata tuwaache wafanye kazi bila ukomo wa muda. Nchini Marekani Jaji hana umri wa kustaafu hadi miaka 80 bado anafanya kazi. Nadhani tuige utaratibu huo.
“Kipindi cha Hayati Baba wa Taifa Mwl. Nyerere hatukuwahi kusikia kauli za Rais ametoa fedha kwa ajili ya hiki au kile, hata kwa mzee Mwinyi sikumbuki kama lilitokea hilo, hilo la Rais ametoa fedha ni la hivi karibuni. Najiuliza, Rais anatoa wapi fedha hizo?
“Kwa mfumo wa Tanzania unaweza kuona Dola na Bunge viko karibu sana. Mtu anakuwa Mbunge akiteuliwa kuwa Waziri au Naibu Waziri anakwenda kwenye Dola huku akiwa bado ni sehemu ya Bunge.
“Bunge linapaswa kila robo tatu ya mwaka iwe inapitia matumizi ya fedha za serikali na kuomba ripoti ya matumizi ya fedha hizo, ikionekana kuna ubadhirifu kwenye matumizi, Bunge limtake Waziri wa Fedha kutoa maelezo na ikibaini kuna uzembe amefanya limuwajibishe.
“Hakuna sehemu yoyote ile kwenye ripoti ya ukaguzi wa hesabu za serikali mwaka juzi kuwa iliandikwa au nilisema Trilioni 1.5 ziliibiwa bali nilitaka kujua matumizi yake, kwa kuwa yalikuwa hayaonekani. Na kimsingi hilo ni tatizo kubwa kuliko hata fedha kuibiwa.
“Bado siamini kama katiba mpya inaweza kutoa suluhisho la mambo yanayolalamikiwa hadi wawepo watu wenye msimamo na taasisi na viongozi wawe na msimamo.Katiba ya wananchi ndiyo Katiba isiwe ya wachache.
“Tanzania ipo uchumi wa Kati lakini mimi siwezi kumudu familia yangu kunywa chai ya maziwa ingawa baba yangu pale Tanga tulimudu kunywa chai ya maziwa enzi hizo. Uchumi lazima uendane na maisha ya wananchi kuwa na mabadiliko hata ya kimaisha,” amesema Prof. Musa Assad.