×

Kiba Awapiga na Kitu Kizito Kichwani

AMEWAPIGA na kitu kizito kichwani! Alisikika mmoja wa mashabiki wa Mfalme wa muziki Bongo, mchezaji mpira na mmiliki wa Lebo ya Kings Music, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ baada ya kuwasikilizisha mastaa na mashabiki wake albam yake mpya inayokwenda kwa jina la Only One King.

Tukio hilo lilijiri usiku wa kuamkia jana kwenye Ukumbi wa Serena Hotel jijini Dar kabla ya albam hiyo kuachiwa jana asubuhi.

Kwa King Kiba ambaye ana miaka zaidi ya 18 kwenye muziki, hii inakuwa albam yake ya tatu baada ya miaka 12 kupita.

Albam yake ya kwanza ilikuwa Cinderella aliyoiachia mwaka 2006 na baadaye mwaka 2009 aliachia album nyingine iliyokwenda kwa jina la Ali K 4Real.

Ndani ya Albam ya Only One King kuna majina ya mastaa wakubwa Afrika na Dunia kwa jumla ambao wameshirikishwa wakiwemo Patoranking, Blaq Diamond, Real Shinski, Khaligraph Jones, Sauti Soul, Sarkodie, King Rudy na wengine kibao.

Tangu mwaka 2021 uanze, King amekuwa akiachia ngoma ‘baki tu baki’ ambazo amewashirikisha wasanii kutoka nje ya nchi na kufanikiwa kutikisa soko la muziki kimataifa.

Katika uzinduzi wa album hiyo mastaa kibao wameonesha kumsapoti Kiba huku maneno yakiwa mengi mtandaoni na mtaani juu ya ujio kiasi cha wengine kudai amewapiga na kitu kizito; Diamond na Harmonize ambao nao wanatikisa soko la muziki, lakini bado hawajaachia albam zao walizotangaza kuziachia kabla mwaka 2021, haujageuka.

Wimbo wake wa Jealous aliomshirikisha staa wa Nigeria, Mayarkun ulimuwekea rekodi mpya Kiba kwa kuwa wimbo uliotazamwa na zaidi ya mara milioni 1 ndani ya saa 12 katika Mtandao wa YouTube.

Pia wimbo huo ulikamata nafasi ya kwanza katika mtandao huo kwa kuwa na watazamaji milioni 6 kwa siku 6 pekee.

Kiba amewahi kuvunja rekodi ya Chibu Dangote na wimbo wake wa Iyo ambao ulifikisha watazamaji zaidi ya milioni 1 kwa saa 13 kunako YouTube.

Japokuwa King Kiba anashikilia rekodi hizo, lakini bado hajafikia rekodi ya Chibu ambaye alifikisha watazamaji zaidi ya milioni 1 kwa saa 8 kupitia wimbo wake wa Waah aliomshirikisha mkongwe wa muziki, Koffi Olomide kutoka Jamhuri ya Kidenokrasia ya Kongo.

Albam yake ya Only One King yenye nyimbo 16 inafanya vizuri katika platforms (majukwaa) za kuuza na kusikiliza muziki.

Katika Mtandao wa Audiomack, kwa jana pekee ilipata zaidi ya wasikilizaji laki moja na elfu tisini.

Kwa upande wa YouTube, wimbo wake wa Bwana Mdogo aliomshirikisha Patoranking ulikuwa kwenye kumi bora za trending za YouTube huku trending namba 11 na 12 zikiwa ngoma zake ndani ya album hiyo.

Ngoma yake ya Oya Oya ambayo tayari ina video yake, hadi jana ilikuwa na watazamaji zaidi ya laki moja kwa muda wa saa 4 pekee.

STORI; BAKARI MAHUNDU, DAR

Leave a Comment