
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amewapongeza Viongozi na wachezaji wa Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu kwa Watu wenye Ulemavu ‘Tembo Warriors’, kufuatia kufuzu kushiriki katika Kombe la Dunia kwa Watu wenye Ulemavu 2022 nchini Uturuki.
“Funzo kubwa ni kwamba ulemavu huu hauzuii kufanya mambo makubwa ndani ya dunia hii, kwa sababu wanasema Mwenyezi Mungu akikupa ulemavu anakupa na mwendo, nani alijua watoto wetu hawa wangeenda mbio kama waliotimia.

“Wanadamu tunachotofautiana ni umbo, lakini maumbile tuko sawa, watu wote tunapiga miayo, tukila chakula tunatoa, uongo? Tuna nyusi na kope, hata wale tunaojiona tumetimia tuna ulemavu wetu, vingine vya siri na vingine vinaonekana, maumbile wote tuko sawa, ambaye ana ulemavu ambaye hana maumbile tuko sawa na maumbile ndio yana m-define mtu.
“Kombe la Dunia ni Kombe la Dunia liwe la kucheza bao ama karata, liwe mpira wa watu wenye ulemavu ili mradi mmeandika historia, hakuna aliyewahi kwenda huko.
“Kuna timu toka wengine hamjazaliwa hapa zipo katika nchi hii ya Tanzania, walishakwenda mashindano ya Dunia? Nilikuwa namtania Waziri Mkuu na Namungo yake, nikamwambia Namungo imeundwa mwaka gani akaniambia 2014, akajisifu wameanza daraja la kwanza, wakaenda Primia wakaenda tukajenga kiwanja wakaenda tukafundisha timu nyingine Kinondoni.
“Nikamwambia lakini hamjaenda mashindano ya Dunia, watoto wangu hawa kesho kutwa wanaenda mashindano ya Dunia, Namungo na hao wengine niliosema toka wengine hamjazaliwa wapo Tanzania wazima, wanabadilishwa tu kila siku,” amesema Rais Samia.