×

Wagombea Ubunge Libya Waitisha Maandamano

WAGOMBEA kadhaa wa ubunge nchini Libya leo wametoa wito wa kufanyika maandamano ya nchi nzima kulaani hatua ya kufutwa kwa uchaguzi wa rais uliosubiriwa kwa muda mrefu na ambao ulipangwa kufanyika Ijumaa.

 

Wengi ya wagombea hao wamesambaza vipeperushi kupitia kurasa za mitandao ya kijamii kuwarai Walibya kuteremka mitaani kupaza sauti na maoni yao juu ya uamuzi wa kufutwa uchaguzi huo rais.

 

Ingawa haijafahamika ni kwa kiasi gani raia wa taifa hilo watajitokeza mitaani, wito huo unadhihirisha kitisho kinachoikabili Libya ambayo bado inaandamwa na mivutano kati ya upande wa mashariki na magharibi.

 

Tume ya Uchaguzi imependekeza uchaguzi wa rais sasa ufanyike Januari 24 lakini hakuna tarehe rasmi iliyopangwa au kukubaliwa na pande hasimu nchini humo.

 

Uchaguzi uliopangwa kufanyika Desemba 25 ulibeba matumaini ya kumaliza muongo mmoja wa kwamo wa kisiasa na machafuko yanayoigubika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika yenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Leave a Comment