
AFISA wa Takukuru anayetoa ushahidi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Lengai Ole Sabaya na wenzake sita ameiambia Mahakama kuwa mshtakiwa huyo anakabiliwa na msururu wa kesi ambazo bado hazijafunguliwa mashtaka.
Akijibu swali la Wakili upande wa utetezi, Sylvester Kahunduka aliyehoji kwa nini katika ushahidi wake, mamlaka imeshikilia pesa za mshtakiwa huyo anayetumikia kifungo cha miaka 30 jela, shahidi amedai kiasi cha pesa kinahusishwa na kesi ambazo hazijafunguliwa.
Ramadhan Juma, shahidi wa 13 upande wa Jamhuri amemaliza kuwasilisha ushahidi wake na kilichokuwa kikifanyika ni maswali ya dodoso.
Hata hivyo, Juma alidai hajui chochote kuhusu pesa za mroso ikiwa ni sehemu ya kiasi kinachoshikiliwa na Mamlaka. Sabaya anatuhumiwa kupokea rushwa ya Sh milioni 90 kutoka kwa Mfanyabiashara Fransis Mroso.
Katika Ushahidi wake wa awali, Juma alidai kuwa Sabaya aligawa kiasi cha fedha alichopokea kutoka kwa Mfanyabiashara huyo miongoni mwa kikundi chake na kiasi kingine alijinunulia gari aina ya Toyota V8 kutoka kwa mfanyabiashara jijini Dar es Salaam siku 10 baada tu ya kujipatia kiasi hicho.
Wakili wa utetezi alihoji ikiwa kuna utofauti kati ya pesa za sabaya zilizoshikiliwa na zile zilizochukuliwa kwa Mroso.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Dk. Patricia Kisinda katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imeahirishwa na itaendelea kusikilizwa Jumatatu Januari 10, 2022.