×

Makamu wa Rais Amuwakilisha Rais Samia Katika Ibada, Anglikana

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango leo tarehe 30 Januari 2022 amemuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika ibada ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu wa nne wa Dayosisi ya Western Tanganyika Askofu Emmanuel Charles Bwatta iliofanyika katika kanisa la Anglikana la mtakatifu Andrea lililopo Kasulu mkoani Kigoma.

 

Ibada hiyo imeongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Maimbo Mndolwa na kuhudhuriwa na maaskofu wa Dayosisi mbalimbali za Kanisa la Anglikana Tanzania na Burundi, Viongozi wa Dini zingine, Viongozi wa serikali, Chama na Wabunge wa mkoa wa Kigoma.

Akitoa salamu za serikali kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan , Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema Serikali ya Awamu ya Sita, inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Kanisa la Anglikana Tanzania, katika kuwahudumia watanzania kiroho na kimwili. Aidha amewapongeza na kushukuru kwa Kanisa la Anglikana Tanzania na Dayosisi zake zote kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwahudumia watanzania tena bila ubaguzi katika huduma za kijamii ikiwemo Elimu na Afya.

 

Makamu wa Rais amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Taasisi zote za dini nchini, ili kuziwezesha Taasisi hizo kuendelea kuwahudumia wananchi kiroho na kimwili kwa ufanisi zaidi. Makamu wa Rais ametoa salamu za pongezi zake na kutoka wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa Askofu Emmanuel Bwatta kwa kuwekwa wakfu na kutawazwa kuwa Askofu wa Nne wa Dayosisi ya Western Tanganyika.

Kufuatia matukio ya mauaji yaliojitokeza siku za hivi karibuni,Makamu wa Rais ameliomba Kanisa la Anglikana Tanzania pamoja na dini zingine kukemea na kutoa mafunzo ya kiroho kwa kufundisha kwa nguvu na mamlaka, maadili mema kwa vijana na watanzania kwa ujumla dhidi ya tamaa ya kujipatia mali haraka kwa njia zisizo halali. Amesema vitendo vya mauaji ni chukizo kwa Mwenyezi Mungu hivyo amewaomba viongozi wa dini kuongoza waumini kufanya toba ya kweli maana kuondokana hali hiyo.

 

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amemsihi Askofu wa Dayosisi ya western Tanganyika kuimarisha ushirikiano baina ya Dayosisi hiyo na dini zingine,serikali na wananchi kwa ujumla ili kuharakisha maendeleo ya kanisa na taifa kwa ujumla.

 

Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa kumaliza na kuondoa kabisa Migogoro katika madhehebu mbalimbali ya dini kwa kuzingatia sheria za Kanisa na miongozo ya imani ya kikristo au dini yeyote husika na taratibu zinazokubalika. Amesema serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi na madhehebu yote ya dini nchini ili kuhakikisha yanafanya kazi kwa amani na utulivu na kwa mujibu wa sheria.

 

Kwa upande wake Askofu wa Dayosisi ya Western Tanganyika Emmanuel Bwatta ameishukuru serikali kwa kuendelea kuimarisha masuala ya ulinzi na usalama hasa katika mkoa wa Kigoma kutokana na kumalizwa kwa vitendo vya uhalifu vilivyokuwa vikitokea wakati wa safari mbalimbali za kufika mkoani Kigoma.

 

Askofu Bwatta ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuboresha sekta ya elimu ikiwemo ujenzi wa madarasa uliofanyika mwishoni mwa mwaka 2021 na ongezeko la wanufaika wa mikopo katika elimu ya juu.

 

Aidha Askofu Bwatta amesema kanisa litaendelea kuungana na serikali katika mapambano dhidi ya Uviko 19 na kuipongeza serikali kwa juhudi zake katika kupambana na ugonjwa huo. Amesema pamoja na malengo makuu ya kanisa ya kuhubiri injili na kutoa mafundisho ya kiroho laki pia kanisa la Anglikana litaendelea kutoa huduma za kijamii kwa manufaa ya wananchi wote.

 

Awali akimkaribisha Makamu wa Rais Kanisani hapo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Mhashamu Askofu Maimbo Mndolwa ameiomba serikali kukamilisha ujenzi wa barabara za kuingia mkoani Kigoma kupitia Uvinza pamoja na ile ya Kakonko Kibondo Kasulu ambazo zimekua na changamoto kubwa kwa muda mrefu. Aidha Askofu Mndolwa ameomba kukomeshwa kwa viongozi wa serikali na wafanyabiashara ambao wamekuwa wakipelekea migogoro ndani ya Kanisa.

 

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango katika ibada hiyo amechangia kiasi cha shilingi milioni tano kwaajili ya Ukarabati wa Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Andrea Kasulu Mkoani Kigoma.

Leave a Comment