×

Kituo cha Taarifa na Maarifa Kilivyoleta Maendeleo na Kuibadili Kipunguni Kutoka Kwenye Ukatili

Mkurugenzi wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Kipunguni, Selemani Bishagazi akitoa elimu kwenye mkutano huo.

 

 

IJUMAA Februari 4 mwaka huu 2022 inaweza kuwa siku ya ukombozi kwa wale waliokuwa wakifanyiwa ukatili wa kijinsia na wasijue pakukimbilia.

Kazi hiyo ilifanywa na Kituo cha Taarifa na Maarifa kilichopo Kipunguni Wilayani Ilala, jijini Dar, maarufu kama Sauti ya Jamii Kipunguni ambacho hivi karibuni kilizindua mradi wa kuchakata mkaa mbadala kwa kutumia taka na kutoa ajira kadhaa kwa wenye uhitaji wa kipato.

Pamoja na mradi huo kikundi hicho kina darasa la kufundisha ushonaji wa nguo za aina mbalimbali, wanatoa elimu ya kulima bustani na mengineyo ambayo yameshawakwamua kimaisha waliofika kituoni hapo kupata ujuzi.

Kinamama wakiufutilia kiumakini mjadala huo.

 

 

Kikundi hicho kilichopo chini ya Mtandao wa Jinsia nchini, TGNP kiliwaalika wakazi wa eneo hilo na wadau wengine kutoka sehemu mbalimbali katika mjadala wa maendeleo na kupinga ukatili wa Kijinsia.

Katika mjadala huo mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Amani Kata ya Kipunguni, Daniel Maragashimba huku TGNP iliwakilishwa na Afisa Program Idara ya Habari, Jackson Malangalila na wenzake.

Wenyeji wa mjadala huo walikuwa ni MKurugenzi wa Kituo hicho, Selemani Bishagazi na Mwenyekiti wake, Fatma Abdulrahman ambao ndiyo walioandaa mjadala huo.

Wakazi wengi maeneo hayo walihudhuria mjadala huo na kuelezea changamoto mbalimbali za ukatili wa kijinsia wanazokumbana nazo huko majumbani mwao.

Afisa Program Kitengo cha Habari TGNP, Jackson Malangalila akitoa elimu kwenye mjadala huo.

 

 

Miongoni wa changamoto zilizoibuliwa na pamoja na wanawake kutohusishwa kwenye umiliki wa mali, watoto kupewa kipigo kisicho stahili kwa makosa waliyoyafanya, ukeketaji, watoto kufanyishwa biashara muda wa masomo, kufanyishwa vibarua vigumu na mengineyo.

Katika mjadala huo wengine walisema kinababa ndiyo wanaoongoza kwa kuwatesa watoto na kinamama ambapo wanawaachia majukumu mengi ya nyumbani.

Kwa upande wa Mary Butiku maarufu kama Mama Chacha yeye kwa upande wake alisema hata wanawake wenzake nao wapo wanaowatesa waume zao kwa kutowapa huduma zao za msingi wanazostahili na kuwasihi waache tabia hiyo.

Mzee Chacha Marwa wa Kipunguni Dar, akiahidi kusambaza elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia katika jamii yake. 

 

 

Mjadala huo ukiendelea mgeni ambaye ni Mwenyekiti wa Amani Kata ya Kipunguni, Daniel Malagashimba alitoa namba yake ya simu na kuwataka waliohudhuria mjadala huo na hata wasiokuwepo wanaposikia tukio la unyanyasaji wa kijinsia kwenye eneo lake wampigie au wafike ofisini kwake kumjulisha ili alifanyie kazi haraka iwezekanavyo.

Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Kipunguni, Selemani Bishagazi katika kusisitiza hilo la kupinga ukatili aliwatajia namba ya simu 116 ambayo ni maalum ya serikali kwaajili ya kupokea taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia ya kuyafanyia kazi.

Watoto wakiwa na bango linaloonesha siku ya kimataifa ya kupinga ukeketaji walipokuwa kwenye mjadala huo.

 

 

Katika mjadala huo wakazi wengi wa maeneo hayo walisema hapo awali kabla ya elimu ya kupinga ukatili kuanza kutolewa na wanaharakati wa Vituo vya Taarifa na Maarifa kulikuwa na matukio mengi ya ukatili wa kutisha lakini sasa hivi baada ya vituo hivyo kusambaza elimu ya kuzuia ukatili wa kijinsia na kuleta maendeleo hali sasa imekuwa angalau.

Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na Maarifa, Sauti ya Jamii Kipunguni, Fatma Abdulrahman akitoa elimu kwenye mjadala huo.

 

 

Baada ya kuingiwa na elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia iliyokuwa ikitolewa kwenye mjadala huo, Mzee Chacha Marwa alisimama na kusema kuanza hapo hatofanya tena ukatili wa kijinsia na kama akithubutu kufanya hivyo basi sheria ichukue mkondo wake haraka dhidi yake.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na wageni kutoka pande mbalimbali akiwemo, Ruth Kipaipai kutoka Loliondo mkoani Arusha ambaye kwa sasa anasomea digrii ya pili ya Master of Applied Social Psychology katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Janeth John kutoka Binti Makini Foundation na maofisa wengine wa Mtandao wa Jinsia nchini TGNP.                                                    MAKALA/PICHA NA RICHARD BUKOS/ GLOBAL PUBLISHERS

Leave a Comment