×

Nabi Amuandaa Djuma Kuwamaliza Mtibwa Sugar

RASMI beki wa pembeni wa Yanga, Mkongomani, Djuma Shaban ataanza kuonekana katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro ikiwa ni baada ya kumaliza adhabu yake ya kufungiwa mechi tatu.

Mkongomani huyo hivi karibuni alisimamishwa kucheza michezo mitatu ya Ligi Kuu Bara na faini baada ya kumpiga kiwiko mchezaji wa Polisi Tanzania.

 

Djuma anamaliza adhabu hiyo baada ya kukosa michezo ya ligi dhidi ya Mbeya City na miwili ya FA ambayo ni Mbao FC kabla ya kumalizia na Biashara United, Jumanne ijayo kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, alisema ameanza kumuingiza beki huyo katika mipango yake ya mchezo ujao wa ligi baada ya kuikosa michezo miwili huku akisubiria dhidi ya Biashara ambao atakuwa anamalizia adhabu yake.

 

Aliongeza kuwa, hivi karibuni alifanya kikao na beki huyo na kumtaka kupunguza jazba za ndani ya uwanja mara baada ya kuchezewa vibaya na wachezaji wa timu pinzani.

“Wachezaji wangu karibia wote wanachezewa vibaya kwa kupaniwa na wachezaji wa timu pinzani, hivyo nisingependa kuwaona wakiwa na jazba mara baada ya kuchezewa vibaya kwa kurudishia.

 

“Nilishamuonya Djuma kutorudishia rafu atakazokuwa anachezewa na wachezaji pinzani kwa hofu ya kupewa adhabu kama aliyoipata ambayo inaigharimu timu katika kupata matokeo mazuri ya ushindi,” alisema Nabi.

 Lunyamadzo Mlyuka, Dar es Salaam

Leave a Comment