
MKUU wa Wilaya ya Meru Eng. Richard Ruyango amewataka wapenzi wa marathon kujitokeza kwa wingi kushiriki Arusha Park Wildlife Marathon inayoandaliwa kufanyika baadaye Novemba mwaka huu.
Eng. Ruyango ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa marathon hiyo ameyasema hayo alipokuwa akitoa zawadi kwa washindi wa marathon ya majaribio iliyofanyika leo katika Hifadhi ya Taifa Arusha.

“Nimefarijika kuona katika zoezi hili la majaribio vijana 70 wamejitokeza. Niwapongeze viongozi wa TANAPA kwa kudhubutu kuanzisha marathon hii. Nimshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anapambana kuhakikisha utalii unarudi na kuendelea kuimarika. Tuendelee kuyatunza, kuyalinda na kuyasimamia vizuri maeneo haya na maliasili zilizomo ili tuweze kurithisha vizazi vijavyo” alisisitiza Mkuu wa Wilaya.
Akielezea upekee wa mbio hizi Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi -Maendeleo ya Biashara TANAPA, Beatrice Kessy amesema uanzishwaji wa mbio hizi ni utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Waziri wa Maliasili na Utalii aliyoyatoa alipotembelea hifadhi ya Taifa Arusha kwa kuwataka wahifadhi kubuni mazao mapya ya Utalii Pia Kamishna Kessy ameelezea utofauti wa mbio hizi kwani zinaanza na kuishia ndani ya hifadhi.

Awali, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi anayesimamia Hifadhi ya Taifa Arusha, Albert Mziray alisema mbio za marathon ni mchezo ambao umepata umaarufu katika siku za karibuni na kwamba Hifadhi ya Taifa Arusha imeiona hii ni fursa ya kuboresha afya za wananchi lakini zaidi kuongeza mapato ya shirika.
“Leo ni uzinduzi wa mbio hizi ambapo tumekuwa na wakimbiaji takribani 70 na tumekimbia kilomita 7. Matarajio yetu ni kwamba hizi mbio zitaingia rasmi kwenye kalenda ya kitaifa na kimataifa baada ya mchakato kukamilika ili mwezi Novemba mwaka huu tuweze kufanya marathon hii.” Alisema Kamishna Mziray.
Kwa upande wake Lomayani Komolo ambaye ni mshirika wa mbio hizi kutoka shirika la Bush 2 Base amesema lengo la marathoni hii ni kutengeneza uelewa kwa jamii kukusu maswala ya Uhifadhi na Utalii pia kuitangaza hifadhi hii ya Arusha ndani na nje ya nchi.
Hifadhi ya Taifa Arusha ni maarufu kwa wanyama jamii ya tumbili kama mbega weusi na weupe, ndege zaidi ya aina 400, pamoja na Mlima Meru wenye urefu wa mita 4,566.