
Siku chache tangu staa wa Bongo Fleva anayeiwakilisha vyema Bongo kimataifa, Diamond Platnumz kuachia video ya ngoma yake mpya ya Gidi, wadau mbalimbali wamejitokeza na kukosoa baadhi ya vipande katika video hiyo.
Miongoni mwa vipande vinavyokosolewa, ni kile kinachomuonesha staa huyo akiwa na bendera ambayo hujulikana kama Confederate Flag ambayo miaka ya nyuma ilikuwa ikitumika na Shirikisho la Majimbo ya Kusini mwa Marekani, inayotajwa kuwa alama ya ubaguzi wa rangi nchini humo ambapo watu weusi hubaguliwa kwa sababu ya rangi ya ngozi zao.
Miongoni mwa waliojitokeza hadharani kumchana Diamond, ni msanii mwenzake Wakazi ambaye kupitia ukurasa wake wa Instagram, amemtaka msanii huyo kukiondoa kipande hicho kabla hakijamletea matatizo katika soko lake la muziki kimataifa hasa nchini Marekani na kwingineko.
Sehemu ya ujumbe wa Wakazi unasomeka: “… Hiyo bendera kwa Marekani ina historia ya kibaguzi na mtu yeyote anayeitumia lazima atawachefua ‘Black Americans’. Sijui ni nani ali-suggest iwekwe ila kiukweli haikuwa idea nzuri…”
Baada ya gumzo kuwa kubwa mitandaoni, Meneja wa Diamond, Sallam SK naye amepost maneno yanayoonekana kuwa kijembe kwa Wakazi na wote wanaokosoa video hiyo kwa kuandika: “Mkiwa na jambo lenu mnanipigia ‘private’, mkitaka kukosoa biashara yangu mnaandika mitandaoni,” ameandika Sallam na kusindikiza na emoji za kucheka.