
Rais Samia Suluhu Hassan amesema minong’ono ya maisha kuwa magumu na vitu kupanda bei, ni kutokana na athari zinazotokana na vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine.
Rais Samia ameyasema hayo leo Machi 8, 2022 wakati akihutubia kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika Viwanja vya Maisara visiwani Zanzibar.
Amesema kuwa mabadiliko ya kupanda bei za bidhaa yanatatoka na na kupanda bei ya mafuta duniani ambazo zinaithiri pia Tanzania.

“Eneo la pili la mabadiliko haya ambalo kidogo limechagizwa na uwepo wa vita hii ya Ukraine na Russia ni kupanda kwa bei za mafuta, mafuta yanapanda bei mno na jinsi mafuta yanavyopanda bei Tanzania hatutonusurika, bidhaa zote zitapanda bei, nauli zote zitapanda bei, kila kitu kitapanda bei” amesema Rais Samia na kuongeza:
“Tumeanza kusikia minong’ono kuwa maisha yanapanda bei, kila kitu kinapanda bei, ni hawa viongozi wetu hawana baraka, hili sio baraka ya kiongozi ni hali ya ulimwengu inavyokenda. Mafuta yanapanda bei duniani na bidhaa zote zitapanda bei” amesisitiza Rais Samia.
Maadhimisho hayo yaliyofanyika visiwani Zanzibar yamehudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi, mawaziri, baadhi ya mabalozi na wawakilishi wa mashirika mbalimbali, pamoja na viongozi wa baadhi ya vyama vya siasa.