

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA MAKAMU WA RAIS
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. PHILIP ISDOR MPANGO, MAKAMU
WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE
HAFLA YA KUPOKEA HUNDI YA GAWIO KUTOKA
KAMPUNI YA AIRTEL TANZANIA
12 APRILI 2022
DODOMA
Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango (Mb.);
Mhe. Nape Nnauye (Mb.); Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari;
Komredi Daniel Chongolo, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi;
Mhe. Anthony Mtaka, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;
Mhe. Jerry Silaa (Mb.), Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma na Waheshimiwa Wabunge Wajumbe wa Kamati yako waliopo;
Ndugu, Emmanuel Tutuba, Katibu Mkuu – Wizara ya Fedha na Mipango;
Prof. Florens Luoga, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania;
Ndugu Mgonya Benedicto, Msajili wa Hazina;
Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma mliopo hapa;
Ndugu Gabriel Malata, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Airtel Tanzania;
Ndugu Dinesh Balsingh, Mkurugenzi Mkuu wa Airtel Tanzania;
Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha, Ofisi ya Msajili wa Hazina na Airtel Tanzania mliopo hapa;
Waandishi wa Habari;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…!
Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kufika hapa kushiriki Hafla hii muhimu ya kupokea gawio kutoka Kampuni ya Airtel.
Pili, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango, pamoja na Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Airtel Tanzania, kwa heshima mliyonipa ya kupokea gawio kwa niaba ya Serikali. Kutoa gawio kwa Wanahisa, kunaashiria kwamba, Kampuni imeendelea kufanya vizuri kiutendaji, na hii inatia moyo na kutoa hamasa kwa Wanahisa.
Tatu, naipongeza Menejimenti na Watumishi wote wa Kampuni ya Airtel Tanzania kwa utendaji wenye tija ambao umeiwezesha kupata faida, kulipa kodi stahiki pamoja na kutoa gawio nono kwa Serikali na Wanahisa wengine. Serikali pamoja na Wanahisa wote katika Kampuni ya Airtel tunajivunia mafanikio makubwa na ya mfano ambayo yametokana na utendaji wenu mzuri wa kazi. Asanteni sana na hongereni.
Waheshimiwa Viongozi, Bodi na Menejimenti ya Kampuni ya Airtel Tanzania;
Hii ni siku nzuri sana kwangu ninaposhuhudia Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache zinafanya vizuri na kulipa gawio (tena kubwa) kwa Serikali na Wanahisa wengine. Kiasi hiki cha gawio cha jumla ya Shilingi bilioni 143 kinachotolewa na Airtel Tanzania kwa Wanahisa wote kwa mwaka 2020/21 ni kikubwa na kitasaidia sana katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo ya nchi yetu.
Nimefahamishwa kuwa kati ya fedha hizo, kiasi cha Shilingi bilioni 88 ni gawio la Serikali kwa mwaka 2020/21 na kuwa katika historia ya uwekezaji wa Serikali katika Kampuni ambazo ina umiliki wa hisa chache (Minority Interest), kiasi hiki hakijawahi kufikiwa na Kampuni yoyote. Hivyo, naipongeza tena Bodi na Menejimenti ya Airtel Tanzania kwa kutekeleza majukumu yake vema na hatimaye kulipa gawio nono Serikalini.
Hata hivyo, pamoja na mafanikio haya mazuri mliyoyapata, ninawataka muongeze juhudi kwa sababu bado kuna wigo wa kufanya vizuri zaidi. Napenda niwahakikishie kuwa Serikali, inathamini na inatambua sana juhudi zenu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Nchi yetu na nawahimiza mwendelee kutimiza wajibu wenu na kuboresha huduma zenu.
Waheshimiwa Viongozi, Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;
Kama mnavyokumbuka, mahusiano ya Serikali na Kampuni ya Airtel Tanzania yalianza mwaka 2001 kupitia Kampuni ya simu ya TTCL na Mobile Systems International Cellular Investments Tanzania BV na Detecon ya Ujerumani. Katika vipindi tofauti tofauti, kumekuwa na mabadiliko mbalimbali ya wabia kwa upande wa mbia mwenza huku Kampuni ikiendeshwa kwa hasara na kugubikwa na matatizo ya kiutendaji na kukosesha wabia gawio. Hata hivyo, kufuatia juhudi za makusudi na mabadiliko ya kimfumo, tumeshuhudia mwenendo chanya wa kiutendaji ambao umepelekea Kampuni ya Airtel kupata faida na hatimaye kutoa gawio kwa Serikali na wabia wengine sambamba na michango maalum. Napenda niwasisitize Bodi na Menejimenti mwendelee kufanya kazi kwa bidii ili Kampuni ya Airtel Tanzania isirudi katika dimbwi la kupata hasara kama ilivyokuwa kabla ya mabadiliko ya kimfumo.
Waheshimiwa Viongozi, Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;
Kama mnavyofahamu, Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Airtel Tanzania tuliingia katika makubaliano maalum ya kiutendaji na kiumiliki ambapo pamoja na mambo mengine, makubaliano hayo yalipelekea umiliki wa Serikali katika Kampuni hii kuongezeka kutoka asilimia 40 kufikia asilimia 49. Aidha, wabia waliingia makubaliano ya kihuduma ya Airtel Tanzania kuilipa Serikali shilingi bilioni 1 kila mwezi kwa kipindi cha miezi 60 kuanzia tarehe 1 Aprili 2019.
Nimefurahi kuona kuwa makubaliano hayo yametekelezwa kikamilifu ambapo, pamoja na mambo mengine, Airtel Tanzania imeendelea kulipa shilingi bilioni moja kila mwezi, na hadi kufikia Machi 2022 jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 36 kilikuwa kimelipwa. Hongera sana Msajili wa Hazina kwa kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa makubaliano hayo. Nawapongeza pia Menejimenti na Bodi ya Airtel Tanzania kwa kutekeleza kwa dhati makubaliano yetu.
Waheshimiwa Viongozi, Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;
Tukio hili la leo linaashiria uwepo wa mazingira mazuri ya kiutendaji na mahusiano thabiti ya kibiashara baina ya wabia. Mapato haya yaliyopatikana yana mchango mkubwa sana katika kugharamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo nchini na kuboresha huduma za jamii ikiwemo afya, elimu na maji kwa Watanzania wote. Hivyo, ni muhimu kuimarisha zaidi utendaji na mahusiano mazuri baina ya wabia ambayo yamepelekea kupatikana kwa gawio na mapato mengine ambayo yanatumika kama chachu ya maendeleo ya nchi yetu ya Tanzania na wananchi wake.
Naelewa kwamba Ofisi ya Msajili wa Hazina inaendelea na kazi ya kupitia kwa undani uendeshaji, umiliki na utendaji wa Mashirika na Taasisi ambazo Serikali imewekeza, hususan Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache, kwa nia ya kuongeza ufanisi. Ninaitaka iendelee kufanya kazi hii kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha kuwa maslahi ya Serikali yanalindwa, kasoro zozote zitakazojitokeza zinaondolewa na Serikali inapata gawio na kodi stahiki kwa uwekezaji wake. Aidha, naitaka pia Ofisi ya Msajili wa Hazina kuendelea na hatua za makusudi za kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kuimarisha Bodi za wakurugenzi pamoja na udhibiti wa matumizi yasiyo na tija.
Serikali ya Awamu ya Sita kwa upande wake itaendelea kuimarisha Ofisi ya Msajili wa Hazina na kuweka mazingira mazuri na endelevu ya kufanya biashara. Hata hivyo, matarajio ya Serikali kwa taasisi nyingine Binafsi ambazo Serikali imewekeza hisa, hata kama ni asilimia 1, ni kuwa zihakikishe zinajiendesha kwa ufanisi na kulipa gawio stahiki Serikalini na kwa Wanahisa wengine.
Waheshimiwa Viongozi, Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;
Jukumu langu hapa leo siyo kutoa hotuba ndefu. Napenda tena kutoa shukrani zangu za dhati kwa niaba ya Serikali kwa Bodi na Menejimenti ya Airtel Tanzania kwa gawio hili walilotoa la Shilingi bilioni 143 kwa Wanahisa wote kwa pamoja. Naipongeza tena Wizara ya Fedha na Mipango na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kusimamia vizuri maslahi ya Watanzania katika Kampuni ambazo Serikali ina hisa. Aidha, kwa umuhimu wa pekee naishukuru sana Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Jerry Silaa (Mb.) kwa ushauri wake mzuri kwa Serikali na usimamizi unaolenga kuhakikisha kuwa uwekezaji wa mitaji ya Umma unakuwa wenye tija. Serikali ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri inaiahidi Kamati ushirikiano wa kutosha.
ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA