
INGAWA wanasema “”kufa ni kufa” lakini kuna vifo vingine huambatana na mateso makali
Jamaa mmoja nchini Kenya aitwaye Caleb Otieno, amepoteza maisha baada ya kuvutwa na mashine ya kuyeyushia vyuma kisha kutupwa kwenye tanuri la moto ambako mwili wake ulipikwa kwenye joto kali.
Otieno alikuwa akifanya kazi katika Kampuni ya Blue Nile Rolling Mills mjini Thika ingawa yeye ni mwenyeji wa eneo la Kogony katika Kaunti ya Kisumu ambapo mabaki ya mwili wake yamezikwa Jumamosi, Aprili 9 mwaka huu.
Mwanaume huyo alikuwa na kibarua cha kuweka vipande vya chuma katika moto mkali na siku ya kufa kwake Machi 25, mwaka huu alikuwa kazini kama kawaida.
Inaarifiwa dakika chache kabla ya kifo chake, alimpa mwenzake fedha ili amnunulie chakula cha mchana.
Mfanyakazi mwenzake aliporudi na chakula hakumkuta Otieno na kwamba wakati akiendelea na kazi alivutwa na mitambo kimakosa na kujikuta akipoteza maisha.
Kamanda wa polisi wa akaunti ndogo ya Thika, Joseph Thuvi aliliambia Gazeti la The Star kuwa, walifika eneo la mkasa na kukusanya chembechembe ambazo zilionekana kuwa vipande vya mifupa kutoka kwenye tanuri hilo.
Inafahamishwa kuwa kampuni aliyokuwa akifanyia kazi marehemu imeahidi kulipa shilingi elfu saba za Kenya kila mwezi kwa miaka mitano kama fidia.