
MWILI wa Msanii wa Bongo Fleva, Maunda Zahir Zorro unatarajiwa kuzikwa kesho Jumamosi kwenye makaburi yaliyopo Kibada, Kigamboni ambako alikuwa anaishi.
Ratiba hiyo ya mazishi imetolewa na muimbaji Banana Zorro ambaye alikuwa kaka mkubwa wa Maunda.
Banana alisema baada ya mdogo wake huyo kufariki, mwili ulihifadhiwa nyumbani kwa baba yao Mzee Zahir Zorro hukohuko Kigamboni.
“Mazishi yatafanyika siku ya Jumamosi (kesho) maeneo ya Kibada kule ambako alikuwa anaishi. Lakini kabla ya hapo mwili ulikuwa hapa nyumbani kwa mzee Zahiri, Kigamboni,” alisema.
Maunda alifariki usiku wa kuamkia juzi Alhamisi Maili Tano kwenda alipokuwa anaishi kufuatia kupata ajali baina ya gari aliyokuwa akiendesha kugongana uso kwa uso na gari ya mchanga.
Maunda aliwahi kutesa kipindi cha nyuma na wimbo wake wa Nifanye Niwe Wako na ngoma zingine kibao, ikiwemo za kushirikishwa.
Na Issa Liponda