
UMOJA wa Mataifa kupitia kwa Naibu Katibu Mkuu wake Gillian Triggs umesema mpango wa kuwapeleka wahamiaji haramu nchini Rwanda kutoka nchini Uingereza ni mpango hatari na unavunja sheria za kimataifa pamoja na sheria za wakimbizi.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza Priti Patel hivi katibuni amesaini mkataba wenye thamani ya kiasi cha Paundi milioni 120 na nchi ya Rwanda kuwapeleka wahamiaji haramu kutoka mataifa mbalimbali ambao wanakimbilia nchini Uingereza kwa ajili ya kujitafutia maisha.
Ndani ya masaa 24 tangu kutangazwa kwa mpango huo Zaidi ya wahamiaji haramu 181 wakiwa kwenye boti sita (6) walizuiliwa baharini wakiwa wanataka kuingia nchini Uingereza, alisema Waziri wa Ulinzi.

Gillian Triggs Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Shirika la kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) amelielezea tukio hilo kuwa halikubaliki hasa wakati huu ambao bado kuna tatizo la kushughulikia wakimbizi kutoka Ukraine.
Mpango wa Serikali ya Uingereza kupeleka wakimbizi na wahamiaji haramu nchini Rwanda umekosolewa vikali na watu na mashirika mbalimbali kuwa ni mpango wa kinyanyasaji lakini pia unavunja usawa wa haki za binadamu.