
MBUNGE wa Jimbo la Mbulu Vijijini kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Flatei Massay ameruka sarakasi Bungeni ikiwa ni ishara ya kuonesha namna ambavyo haridhishwi na utendaji kazi na ahadi za Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kutoa ahadi ambazo hazitekelezeki katika Jimbo lake ikiwa ni sambamba na kujenga barabara ya Lami kutoka Mbulu hadi Haydom.
Mbunge huyo ameruka sarakasi wakati akichangia hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka 2022/2023.
Flatei amesema ingawa aliahidiwa ujenzi wa barabara hiyo tangu katika bajeti ya mwaka jana, Kamati ya Bunge ya Miundombinu imetoa ripoti kuwa fedha zilizotengwa mwaka jana zimepelekwa kulipa madeni.
Mbunge huyo ambaye alikuwa anaongea kwa msisitizo alinukuliwa akisema:
“Kama waliniahidi kuwa barabara itajengwa hilo tangazo linachukua muda gani? Mimi hapa mheshimiwa Spika sio shilingi tu. Mimi wananchi wameniambia shilingi niichukue niende nayo Mbulu Vijijini maana hapa hamna namna tena.”

Mbunge Flatei alimhoji Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kama hamtoi nje ya ukumbi wa Bunge basi apige sarakasi.
“Mimi naona wanataka kunitengenezea ajali kuliko kukitengenezea ajali chama changu si bora uruhusu tu niruke hapa ili wastuke sasa nitafanyaje sasa,”amesema.
Mwisho kabisa Mbunge huyo alimtaka na kumsihi Profesa Makame Mbarawa ambaye ni Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuhakikisha anajenga barabara hiyo kwa kiwango cha Lami asipofanya hivyo ni ama zake.