
MATOKEO rasmi yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi yanaonesha mwanasiasa mkongwe nchini Kenya, Raila Odinga, akiongoza kwenye mbio za kuwania urais, huku ya Reuters yakimuweka William Ruto nafasi ya juu.
Matokeo rasmi yaliyotangazwa Jumamosi na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC)yanaonesha mwanasiasa mkongwe nchini Kenya, Raila Odinga, akiongoza kwenye mbio za kuwania urais, huku ikiwa ni asilimia 26 tu ya kura zilizohisabiwa tangu uchaguzi kumalizika siku tano zilizopita.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyowekwa kwenye ubao wa IEBC katika ukumbi wa Bomas of Kenya jijini Nairobi, Odinga mwenye umri wa miaka 77 alikuwa na 54% ya kura mbele ya Naibu Rais William Ruto mwenye 45% kufikia mchana wa Jumamosi Agosti 13, 2022.
Kenya, inayoongoza kwa kuwa na uchumi mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na demokrasia inayoshamiri, ilifanya uchaguzi wa urais, ubunge na ugavana siku ya Jumanne Agosti 9, 2022.
Ruto na Odingawanaonekana kuchuana kwenye kinyang’anyiro cha kumrithi Rais Uhuru Kenyatta, ambaye ametimiza ukomo wa mihula miwili madarakani.
Kenyatta alikosana na aliyekuwa mshirika na naibu wake, Ruto, mara tu ya uchaguzi wa mwisho wa mwaka 2017 na tangu hapo amekuwa akimsogeza Odinga karibu yake na hatimaye kumuunga mkono kwenye uchaguzi huu.