
KOCHA wa Manchester United Erik ten Hag anafikiria wazo la kumuacha Nahodha Harry Maguire wakielekea kuwavaa Liverpool siku ya Jumatatu.
Maguire alianza katika mechi zote mbili ambazo za United walichezea kichapo dhidi ya Brighton na Brentford na beki mpya wa kati Lisandro Martinez akitolewa baada ya mapumziko nafasi yake ikichukuliwa na Raphael Varane United ikibugizwa mabao 4 kwa sifuri.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa Ten Hag anatafakari juu ya uwezekano wa kumuanzisha Martinez na Raphael Varane ambaye ataanza kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha United msimu huu.

Habari za ndani kutoka katika timu ya Manchester United zinasema baadhi ya wachezaji wa United wanahisi mbinu za Ten Hag haziendani na aina yao ya uchezaji na wangependelea Ten Hag abadilishe namna ya uchezaji watakapokutana Liverpool siku ya Jumaatau.
Inakumbukwa Liverpool waliwazaba United kwa mabao 5-0 katika uwanja wa Old Trafford msimu uliopita na kuwachabanga 4-0 Anfield miezi sita baadaye.

Maguire, 29, alishawahi kuwekwa benchi na kocha wa muda aliyepita Ralf Rangnick kwenye mechi dhidi ya Arsenal mwezi wa Aprili wakati United ilipofungwa 3-1, lakini mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza ameendelea kuwa nahodha wa timu hiyo chini ya Ten Hag, licha ya ming’ono mingi inayoshinikiza Maguire kuvuliwa kitambaa hicho cha unahodha.
Imeandikwa: Abdallah Kaputi kwa msaada wa mitandao.