
TAKRIBANI watu 21 wamefariki dunia na wengine 30 kujeruhiwa baada ya tetemeko la ardhi kupiga katika Mji wa Kangding uliopo katika Jimbo la Sichuan lililopo Kusini Magharibi mwa China.
Watu hao walifariki maeneo tofauti ambapo watu 14 walipoteza maisha katika kaunti ya Sichuan ya Shimian na saba walifariki katika Jimbo lililopo karibu na eneo la Luding nchini humo.
Shirika moja la habari nchini humo limesema tetemeko hilo lilifanya uharibifu mkubwa katika mji mmoja wa nchi hiyo ambapo umesababishwa na maporomoko ya ardhi ya milimani.
Shirika hilo limeeleza kuwa barabara ya kuelekea mji mwingine ilifungwa huku njia za mawasiliano katika maeneo ya makazi ya zaidi ya watu 10,000 zikizuiwa.

Tetemeko hilo linaukubwa wa 6.6 katika kipimo cha Richter ambapo lilisambaa hadi umbali wa kilometa 43 na kuharibu majengo pamoja na kuyaacha maeneo mengine bila nishati ya umeme.
Aidha, tetemeko hilo lilitikisa majengo yaliyopo katika Mji Mkuu wa Chengdu ambapo mamilioni ya watu wamefungiwa nyumbani wakiwa chini ya vizuizi vikali vya kukabiliana na virusi vya Corona.

Mamia ya waokoaji wametumwa kwenda eneo ambalo ni kitovu cha tetemeko hilo huku wafanyakazi wengine wakijaribu kusafisha barabara zilizozuiwa na vifusi vya udongo ulioporomoka kutoka milimani.
Imeandaliwa na Sanifa Khalifa kwa msaada wa mtandao