
HAYATI Malkia Elizabeth II wa Uingereza jeneza lake leo Septemba 14, 2022 limewasili Ukumbi wa Westminster, London ambapo atawekwa hapo katika bunge. Jeneza hilo lilotokea Kasri ya Buckingham.
Mfalme Charles III na wanawe, Wanamfalme William na Harry, wametembea nyuma ya jeneza la Malkia Elizabeth II kuelekea katika Westminster Hall, ambako Malkia atatazamwa na umma kwa siku nne, kabla ya kuzikwa.
Ndugu zake Mfalme, Binti mfalme Anne, Mwanamfalme Andrew na Mwanamfalme Edward pia walitembea katika maandamano ya huzuni kupitia katikati mwa London.

Umati mkubwa wa watu wamejitokeza katika barabara huku maelfu ya watu wakitarajiwa kusafiri kwenda Westminster kutoa heshima zao.
Gwaride hilo litafanyika huku kukiwa na ufyatuaji wa bunduki kwenye eneo la Hyde Park na kupigwa kwa kengele ya Big Ben ya bungeni.

Mwili wa Malkia utalazwa kwa siku nne katika Ukumbi wa Westminster wa karne 11. Ukumbi huo utakuwa wazi kwa saa 23 kila siku kwa ajili ya wageni na utalindwa na wanajeshi kutoka nyumba ya kifalme.

Elizabeth alifariki Septemba 8 huko katika Makazi ya Balmoral katika eneo Scottish Highlands, sehemu ambayo Malkia aliipenda na ndipo Charles alipokuwa mfalme.

Mazishi ya malkia yamepangwa kufanyika Septemba 19 huko Westminster Abbey. Jeneza hilo baadae litachukuliwa kwenda Windsor kwa ajili ya ibada ya mazishi, ambapo mume wa malkia, Prince Philip, ndipo alipozikwa mwezi Aprili 2021.